Ligi Kuu

Leo ni vita ya mpangaji na mwenye nyumba

DAR ES SALAAM: NYASI za Uwanja wa KMC uliopo Mwenge zitawaka moto wakati mmiliki wa dimba hilo KMC FC watakapoikaribisha Yanga ambao wanautumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani.

Kuelekea mchezo huo Kocha wa Yanga, Hamdi Miloud amesema katika mchezo uliopita walipata matokeo yasiyoridhisha dhidi ya JKT Tanzania hivyo wanataka kubadilisha hali katika mchezo wa kesho.

“Kwa upande wangu, mchezo dhidi ya JKT Tanzania ulikuwa wa kwanza nikiwa Yanga, ningependa kushinda mchezo wa kwanza lakini tulitoka sare, tumejiandaa kiakili, kuhakikisha tunapata ushindi na kuepuka kuvunja mioyo ya mashabiki wetu, sisi wote, benchi la ufundi na wachezaji, tunatamani sana kushinda mchezo wa kesho,” amesema.

Miloud amesema anakubaliana na mashabiki wana kila sababu ya kutoridhika kwa sababu Yanga klabu kubwa na mashabiki wanataka kushinda kila mchezo.

“Kesho tutafanya kila tuwezalo kushinda mchezo huu kwa sababu tunahitaji alama tatu, ninataka kuwapa ujumbe mashabiki wetu kwamba tunapambana na kufanya kazi kwa bidi kwa ajili yao na wachezaji wanajua wanachopaswa kufanya kesho na pia katika siku zijazo.

Tuko hapa kushinda mataji, hatuko hapa kwa ajili ya kazi tu, mashabiki wasikata tamaa kwa sababu ya sare moja bado tuna michezo mingi ya kucheza, kila kitu kinawezekana bado hatujachelewa, tuna muda lakini lazima tufanye kila tuwezalo kushinda michezo yote ili kuwapa furaha mashabiki wetu kwa sababu wao wako pamoja nasi,” amesema.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa KMC FC, Kali Ongala, amesema maandalizi ya mchezo yako vizuri, wanaifahamu timu wanayokutana nayo na wanaenda kupambana kutafuta alama muhimu.

“Tunawaheshimu Yanga, timu kubwa, safu ya ushambuliaji iko vizuri wanafunga mabao memgi, tumejiandaa kwa ajili ya kuzuia haitakuwa mechi rahisi tunaenda kupambana hadi  dakika 90 ziishe.

“Wana wachezaji wakubwa lakini kwa siku chache tumefanya maandalizi mazuri na tupo tayari kwa matokeo yoyote yatakayotokea tutayapokea,” amesema.

 

Related Articles

Back to top button