Tetesi

“Kwa Pacome ogopa matapeli” – Ally Kamwe

DAR ES SALAAM: OGOPA matapeli ni kauli ya Afisa habari wa Yanga, Ally Kamwe baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa kiungo wao Pacome Zouzoua yupo sokoni na Al Ahly wameweka dau.

Taarifa hiyo imezua taharuki kwa mashabiki wa klabu hiyo wakihofia kiungo huyo kuondoka ndani ya kikosi hicho hali ya kuwa msimu uliopita ameonyesha uwezo mkubwa.

Baada ya taharuki hiyo kwa mashabiki, Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe ametoa kauli kuwa nyota huyo hauzwi na wapo kwenye mazungumzo ya kumuongeza mkataba.

“Huo ni uzushi na uongo kuwa Pacome anaondoka Yanga, hakuna ofa iliyofika mezani kwetu, tulikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na mazungumzo yanafanyika kuongeza mwingine kusalia ndani ya kikosi,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa jitihada kubwa inaendelea kufanyika kwa sababu malengo yao ni kucheza nusu na fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Hatufikirii kuacha mchezaji yoyote aliyekuwa kwenye mipango ya kocha Gamondi akiwemo Pacome. yupo kwenye mikakati yetu kuelekea msimu ujao wa mashindano,” amesema Ofisa huyo.

Kamwe amesema wananchi wanatakiwa kutulia na kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki ambacho wapo kwenye mchakato wa kutangaza wachezaji wapya na wanaongezewa mkataba.

Related Articles

Back to top button