
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerson Msigwa kuanza mchakato wa kuusajili Uwanja wa Benjamini Mkapa, sehemu ya kukimbia riadha, kwenye Shirikisho la Dunia la mchezo huo.
Kabudi amezungumza hayo katika ziara yake kwa mara kwanza tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuongoza wizara hiyo, alipotembelea ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kukagua ujezi unaoendelea wa Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Amesema ameridhishwa na ukarabati wa baadhi ya maeneo ya uwanja huo ikiwemo sehemu ya kukimbia (Riadha) na kuwataka katibu na watu wake kuchukua hatua ya kusajili eneo hilo katika shirikisho la mchezo huo kwa ngazi ya kimataifa.
“Kwa Afrika Mashariki na Kati, Benjamini Mkapa umetakiwa kuwa na viwango bora hasa katika eneo la kukimbia riadha naagiza sehemu hii ya uwanja isajiliwe katika shirikisho husika la dunia.
Ukarabati wa maeneo mengine unaendelea kuinua viwango na hadhi kwa Afrika Mashariki na Kati, tayari kumewekwa nyasi asilia katika eneo la kuchezea (Pitch) awali ilikuwa Plastic, zilikuwa zinawaumiza wachezaji,” amesema.
Kabudi amesema Taifa hili limepiga hatua kubwa, huku akieleza kuwa ameridhishwa na ukarabati mkubwa unaoendelea na pia ametoa maelekezo kuhakikisha uwanja huo unamalizika mapema kabla ya wakaguzi kutoka CAF kuwasilini nchini.
“Tuna uwenyeji wa mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027, tunalazimika kumaliza uwanja mapema, kuna viti vipo bandarini na tunategemea hadi Februari viti 60,000 vitakuwa vimewasili na kuanza kufungwa,” amesema.