Kesi ya uhujumu uchumi ya Nicole Berry kuunguruma mahakamani Mei 13

Dar es Salaam: KESI ya uhujumu uchumi inayomkabili msanii maarufu wa uigizaji, Joyce Mbaga (32), anayefahamika kwa jina la kisanii Nicole Berry, pamoja na mwenzake Rehema Mahanyu (31), imetajwa tena jana, Jumatatu, Machi 14, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni.
Katika kikao hicho, upande wa Jamhuri uliwasilisha ombi la kuongezewa muda kwa sababu upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Mahakama iliridhia ombi hilo na kupanga kesi hiyo kutajwa tena Mei 13, 2025, saa tano asubuhi.
Washtakiwa hao kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Machi 10, 2025, ambapo walisomewa mashitaka matatu ya uhujumu uchumi, likiwemo la kuongoza genge la uhalifu.
Mashitaka hayo yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira, na Wakili wa Serikali, Rhoda Maingu.
Inadaiwa kuwa makosa hayo yalitendeka kati ya Julai 2024 na Machi 2025 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha, Machi 17, 2025, mshtakiwa wa kwanza, Nicole Berry, aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa.
Alidhaminiwa kwa hati ya nyumba yenye thamani ya Shilingi milioni 100, iliyotolewa na mmoja wa wadhamini wake ambaye jina lake halikuwekwa wazi.