Taifa Stars Afcon 2025 ileee!

KIKOSI cha Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kinashuka dimbani leo wakiwa na matumaini ya kutafuta pointi mbele ya wenyeji wao, DR Congo, mchezo wa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2025).
Mchezo huo unaochezwa kwenye Uwanja wa Marty’s (Stade Marty’s) nchini, DR Congo, saa 1:00 Usiku .
Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Selemani ‘Morocco’, amesema wachezaji wapo tayari, na wana matarajio makubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wa leo.
“Tunawaheshimu Congo, wana timu nzuri, hii mechi ni kama dabi kwa sababu kila mmoja nahitaji kutafuta alama tatu, lazima tupambane tushinde hii mechi,” amesema Morocco.
Ameongeza kuwa wachezaji hawana ‘presha’ na wanahitaji kupata matokeo chanya katika mechi hiyo na baadae wanaenda kutafuta alama tatu za nyumbani.
Nahodha wa Stars Himid Mao amesema “Tuna nguvu tunaasilimia kubwa kupata ushindi ugenini, tunaheshimu Congo wako nyumbani lakini watambue sisi watanzania tumekuja kutafuta alama tatu, hatubweteki,” amesema Himid.
Hadi sasa Taifa Stars ina alama nne baada ya michezo miwili huku Congo wakiwa na alama sita baada ya kushuka dimbani mara mbili.