Kaseba amtaka Mwabaka kutetea mabondia

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI anayemaliza muda wake wa Chama cha Mabondia wa Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBA), Japheth Kaseba, amemtaka mwenyekiti mpya wa chama hicho, Kisua Mwabaka, kuwa tayari kukabiliana na lawama na upinzani katika kutetea maslahi ya mabondia nchini.
Kauli hiyo imekuja baada ya Mwabaka kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TPBA katika uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam, chini ya usimamizi wa maofisa wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Katika uchaguzi huo, Ajemi Amani alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu, huku wajumbe waliochaguliwa kuwa ni Mariana Msabila, Nawawi Ahmad na Mohamed Jaylan.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Kaseba amesema Mwabaka amepewa dhamana na mabondia wenyewe, hivyo anapaswa kuhakikisha anatanguliza maslahi yao kuliko jambo lolote lingine.
“Lazima ategemee lawama, ategemee kuchukiwa na hata kutengwa, lakini ahakikishe anasimamia haki za mabondia na kuwatetea wakati wote,” amesema Kaseba.
Amesema mchezo wa ngumi za kulipwa una changamoto nyingi na kuna watu ambao wamekuwa wakinufaika na jasho la mabondia, jambo linalohitaji viongozi wenye ujasiri na msimamo wa kuwalinda wanamichezo hao.
Kaseba alibainisha kuwa moja ya majukumu makubwa ya uongozi mpya ni kuhakikisha mabondia wanapata mafanikio na kutambua haki pamoja na wajibu wao ndani ya mchezo huo.
Pia, amezungumzia umuhimu wa viongozi hao kuweka mikakati ya kuwainua mabondia waliowahi kufanya vizuri lakini wakaporomoka katika viwango vyao, na kuwasaidia mabondia chipukizi ambao bado hawajapata nafasi ya kutambulika.
Amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa mabondia kuhusu masuala mbalimbali ya taaluma yao na kuwahamasisha wanamichezo wengine kujiunga na chama hicho ili kuongeza umoja na kuibua vipaji vipya vitakavyokuza mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.



