Mastaa

Kajala: “Ni lini nilitangaza kuachana naye?”

DAR ES SALAAM: MREMBO kutoka tasnia ya filamu za Bongo Movie, Frida Masanja ‘Kajala’, amewajibu baadhi ya mashabiki walioibua mjadala kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi, baada ya kumuweka wazi mpenzi wake mpya mitandaoni huku akiwa amemficha sura.

Kajala amewataka mashabiki na watu wanaofuatilia maisha yake binafsi kumuacha aishi maisha yake, akisisitiza kuwa hajawahi kutangaza rasmi kuachana na mpenzi ambaye baadhi ya watu wamekuwa wakimhusisha naye.

Kupitia majibu yake kwa mashabiki, Kajala amehoji sababu za watu kudhani kuwa ameachana na mpenzi huyo, akisema:

“Walimwengu nyie, kwani ni lini niliwahi kutangaza kuachana na huyo mnayemsema? Halafu kwa nini mhisi nimempost huyo? Niacheni na maisha yangu.”

Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya mashabiki kumfuata kwenye mitandao ya kijamii na kudai kuwa huenda bado hajaachana na msanii Harmonize, kufuatia picha ya mwanaume aliyemuweka mtandaoni bila kuonyesha sura yake.

Aidha, Kajala ameonekana kukerwa na madai yanayosambazwa kuhusu maisha yake ya kimapenzi, akiendelea kuhoji ni wapi alipowahi kutoa kauli ya kutangaza kuachana na mtu huyo.

“Ebu acheni… Wapi nilisema hayo maneno? Naomba mnikome,” amesema Kajala.

Hata hivyo, licha ya mjadala huo kuibuka mitandaoni, Kajala hajatoa kauli ya moja kwa moja kuhusu uhusiano wake na Harmonize katika maelezo yaliyotolewa, huku madai ya kuachana yakibaki kuwa sehemu ya mijadala ya mashabiki.

Kwa sasa, kitendo cha Kajala kumuweka mtandaoni mwanaume huyo huku akificha sura yake kimeendelea kuibua maswali miongoni mwa mashabiki kuhusu maisha yake ya kimapenzi.

Related Articles

Back to top button