Foden arejea kwa kishindo, wakiitandika Athens 5-1

MANCHESTER: KIUNGO wa Manchester City, Phil Foden ameonesha kiwango cha juu mno jana Jumanne akifunga mabao matatu wakiichapa AEK Athens, akiisaidia timu hiyo kurejea kwenye njia ya ushindi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
City ilihitaji kujibu mapigo baada ya kufungwa 4-2 nyumbani na mabingwa watetezi Paris St-Germain wiki iliyopita, na walifanya hivyo kwa namna bora zaidi wakiitawala mechi hiyo waliyoshinda mabao 5-1.
Elliot Anderson alifunga bao la kuongoza ikiwa ni muda mfupi baada ya mchezaji mwingine mpya, Enzo Fernandez, kupiga mpira wa adhabu uliogonga mwamba wa juu.
Foden, ambaye wikiendi iliyopita alifunga bao lake la kwanza tangu mwezi Desemba, alifunga tena na kuipatia City bao la pili, akipokea pasi kutoka kwa Rico Lewis kabla ya kupiga shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni.
Athens hawakuonesha tishio lolote katika kipindi cha kwanza, lakini walijibu mapigo dakika saba baada ya kipindi cha pili kuanza, pale beki wa pembeni Stavros Pilios alipofunga kwa shuti la kwanza la timu yake kulenga lango.
Hata hivyo, dakika chache baadae Foden alimtengenezea nafasi Rayan Cherki ambaye alifunga kwa ustadi, kabla ya kiungo huyo wa Uingereza kupiga shuti la moja kwa moja lililoingia wavuni, kabla ya kukamilisha mabao yake matatu kwa kufunga kutoka karibu na lango dakika 11 baadae.
Kwa matokeo hayo, City sasa inashikilia nafasi ya sita ya msimamo wa Ligi ya Mabingwa, ikiwa na pointi sita baada ya mechi tatu.
Nafasi ya tano ipo Barcelona na piointi zao sita, sawa na Aston Villa wanaoshika nafasi ya nne wakati Stuttgart ikiwa ya tatu kwa pointi saba huku Liverpool na vinara PSG wakiwa wamefungana kwa pointi tisa.




