Filamu

ZIFF, EU wafungua milango kwa wasanii filamu

DAR ES SALAAM: WASANII wa filamu nchini wamehimizwa kutumia maonesho ya tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF), kubadilishana mawazo, kujifunza kutoka kwa wadau wa kimataifa na kujenga mahusiano yatakayosaidia kukuza kazi zao na tasnia ya filamu kwa ujumla.

Akizungumza na Spotileo Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa onesho la filamu ya A Land Apart ya Nigeria jana usiku Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale, amesema maonesho hayo yanatoa nafasi kwa watengenezaji wa filamu kukutana, kujadili kazi zinazowasilishwa na kupata mitazamo mipya kuhusu utengenezaji wa filamu.

Mwale amewataka watengenezaji wa filamu wa ndani kujitokeza kushiriki mijadala na kutumia fursa hizo kujifunza kuhusu mada na mbinu mbalimbali zinazoweza kuboresha kazi zao.

Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Jean Marc Pisani, amesema tasnia ya filamu ni muhimu si tu katika kuunganisha tamaduni za Afrika na Ulaya, bali pia katika kukuza uchumi na kufungua fursa kwa vijana.

“Tasnia ya filamu ina nafasi muhimu katika kukuza uchumi na kufungua fursa kwa vijana, hususan wanaoishi mijini, kupitia ubunifu, uzalishaji wa kazi za sanaa na shughuli zinazohusiana na tasnia hiyo,”amesema.

Pisani amesema mpango huo unaungwa mkono na nchi 10 wanachama wa EU zilizopo Tanzania, akieleza kuwa filamu ni sekta inayoweza kunufaisha vijana wenye vipaji vya uandishi, uongozaji na utayarishaji wa kazi za sanaa.

Maonesho hayo yataendelea Bagamoyo, mkoani Pwani, Oktoba 27, 2026, ambapo filamu ya makala Techplomacy itaoneshwa katika ukumbi wa TASUBA Bagamoyo.
Mwisho

Related Articles

Back to top button