Hansi Flick: Tuna cha kujifunza kwa PSG

PARIS: BAADA ya kichapo cha mabao 4-2 walichopata dhidi ya Paris Saint-Germain katika Ligi ya Mabingwa jana Jumanne, Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, amesema timu yake ina mengi ya kujifunza kutokana na hilo.
Tangu kuanza kwa msimu hii ni mara ya kwanza Barcelona inapoteza mchezo, baada ya kuanza kampeni hiyo kwa kiwango cha juu mno.
Flick amekiri ulikuwa mchezo mzuri, lakini akaongeza kuwa mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa ni timu bora zaidi kwa sasa.
“Ulikuwa mchezo wa kuvutia sana. Mwishowe, PSG walionyesha kuwa wao ni timu bora kuliko sisi. Tumepoteza mchezo huu, lakini tumejifunza mengi kutokana kwao.
“Wana ubora mkubwa wanapobadilisha mchezo kutoka ulinzi kwenda kushambulia. Tulijaribu kujilinda dhidi yao na tulifanya vizuri, lakini katika dakika 15 za mwisho hatukuwa na nguvu za kutosha.
“Hii si kisingizio lakini maandalizi ya mchezo huu hayakuwa bora zaidi, lakini sasa tunapaswa kuchambua kilichotokea. Tunahitaji kufanya vizuri zaidi hapo baadaye, ingawa pia kulikuwa na mambo tuliyoyafanya vizuri sana,” alisema Flick.
Mabao ya PSG kupitia kwa Desire Doue na Lucas Hernandez yalifutwa na mabao kutoka kwa kinda Xavi Espart na Lamine Yamal, ambaye alikuwa katika kiwango cha juu.
Hata hivyo, dakika chache baadae, Vitinha aliirejeshea PSG uongozi kabla ya dakika tano baadae Fabian Ruiz kuhitimisha ushindi huo kwa bao la nne dakika ya 86.
Barcelona ambao ni vinara wa La Liga, wanarejea nyumbani kuanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wa El Clasico dhidi ya Real Madrid utakaochezwa Jumapili hii, Uwanja wa Camp Nou.




