Nyumbani

Azam FC: Chamazi mara 1001, tunataka makundi

DAR ES SALAAM: AZAM FC imesema inalenga kufanya vizuri zaidi ya ilivyofanya msimu uliopita katika Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo katika mchezo wa marudiano dhidi ya ZED FC ya Misri.

Ofisa Habari wa Azam FC, Hashim Ibwe, amesema kikosi hicho kinaamini kina uwezo wa kufuzu hatua ya makundi kwa mara nyingine na kulinda heshima kilichojijengea katika mashindano hayo msimu uliopita.

Ibwe amesema maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri huku wachezaji wakiwa tayari kupambana kuhakikisha wanapata ushindi katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Amesema kauli mbiu ya “Chamazi mara 1001” inalenga kuhamasisha mashabiki na kuongeza morali ya timu katika harakati za kutafuta nafasi ya kucheza hatua ya makundi.

“ Sisi ni zaidi ya ZED, tuko nyumbani na tunaweza kufanya kile tulichokifanya msimu uliopita, kucheza hatua ya makundi kwa mara nyingine tena. Tunaweza kulinda heshima tuliyoweka msimu uliopita, ndiyo maana tukasema Chamazi mara 1001,” amesema Ibwe.

Ibwe amesema wachezaji wako tayari kupambana na kupata ushindi, huku akiwahimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi Oktoba 24 ili kuipa timu nguvu ya kufanikisha lengo hilo.

Azam FC inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 dhidi ya ZED FC katika mchezo wa kwanza uliochezwa Cairo, Misri, Oktoba 16, mwaka huu.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kuhitaji ushindi katika mchezo wa marudiano ili kuongeza nafasi ya kusonga mbele na kuendelea na harakati za kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Related Articles

Back to top button