JKT Queens yakumbana na adhabu nzito

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Soka la Wanawake imeitoa adhabu mbalimbali kwa viongozi, wachezaji na waamuzi kufuatia matukio yaliyojitokeza katika michezo ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL), huku JKT Queens ikiwa miongoni mwa timu zilizoathirika zaidi.
Katika kikao kilichofanyika Dar es Salaam, kamati hiyo ilipitia taarifa za mchezo namba 95 kati ya Mashujaa Queens na JKT Queens na kubaini ukiukwaji wa kanuni mbalimbali.
Mwanasaikolojia wa JKT Queens, Naomi Kaniki, amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi sita na kutozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kuwashambulia viongozi wa timu pinzani.
Kwa upande wa wachezaji, Najath Abass amefungiwa michezo sita na kutozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kumshambulia mwamuzi msaidizi wa mchezo huo pamoja na dereva wa timu ya Mashujaa Queens.
Naye Winfrida Gerald amefungiwa michezo sita na kutozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kumshambulia mwamuzi msaidizi, huku ikielezwa kuwa ni kosa la kujirudia.
Wachezaji Donisia Minja na Alia Fikiri wamefungiwa michezo mitatu kila mmoja na kutozwa faini ya Sh 500,000 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia mwamuzi msaidizi katika mchezo huo.
Katika hatua nyingine, Mratibu wa mchezo Fatuma Kitamuyo amepewa onyo kali na kufungiwa kusimamia shughuli za mpira wa miguu kwa miezi mitatu kutokana na kushindwa kuwasilisha taarifa kamili ya matukio ya ukiukwaji wa kanuni yaliyojitokeza katika mchezo huo.
Aidha, mwamuzi wa mchezo huo, Amina Kyando, ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wanaochezesha kwa muda kutokana na kosa la kutowasilisha taarifa sahihi katika ripoti yake.
Wakati huo huo, Kamati hiyo ilijadili mchezo namba 109 wa Ligi Kuu ya Wanawake kati ya JKT Queens na Ruangwa Queens uliokuwa upigwe Mei 27, 2026 katika Uwanja wa Isamuhyo, Dar es Salaam.
Kamati ilibaini kuwa Ruangwa Queens iliwasilisha ombi la kuahirisha mchezo huo muda mfupi kabla ya kuanza wakati maandalizi yote ya mchezo yalikuwa yamekamilika.
Kutokana na hali hiyo, JKT Queens imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kwa mujibu wa kanuni husika, huku Ruangwa Queens ikipokwa alama tatu kwenye msimamo wa ligi.
Pia, Mwenyekiti wa Ruangwa Queens, Yusuph Mpame, amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na timu yake kutofika uwanjani kucheza mchezo huo.




