Yanga yamuenzi Aisha Masaka kwa tuzo ya heshima

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Klabu ya Yanga umeonesha kuthamini mchango wa wachezaji wake wa zamani kwa kumpa tuzo ya heshima mshambuliaji wa zamani wa timu yao ya wanawake, Aisha Masaka, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Brighton & Hove ya nchini Uingereza.
Aisha Masaka alionesha uwezo mkubwa akiwa na Yanga Princess kabla ya kupata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Uwezo wake uliwavutia waajiri wake wa sasa na kumfungulia milango ya mafanikio kimataifa.
Tuzo hiyo ilitolewa Jumatano, Mei 21, katika hafla maalum iliyoandaliwa na klabu ya Yanga kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa wachezaji wa timu ya wanawake, Yanga Princess, mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Mbali na Masaka, wachezaji wengine waliotunukiwa tuzo kwa mafanikio binafsi ni pamoja na:Aregesh Kalsa, aliyepata tuzo ya Goli Bora la Msimu baada ya kufunga bao la kuvutia dhidi ya Bunda Queens.
Rita Akarekor, aliyetunukiwa tuzo ya Mchezaji Mwenye Nidhamu kwa kuonesha nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja. Mukandayisenga Jeanine, ambaye aliibuka Mfungaji Bora wa Msimu kwa mabao 16 – 13 katika Ligi Kuu na 3 katika mashindano ya Samia Cup.
Angela Michael, aliyepokea Tuzo Maalum kwa mchango wake muhimu kwenye timu.Uzoamaka Igwe, ambaye alinyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu kutokana na kiwango bora alichokionyesha msimu mzima.
Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Arafat Haji, alisema kuwa kuandaa tuzo hizo ni hatua muhimu ya kihistoria kwa timu ya wanawake ya Yanga na ni ushahidi wa dhamira ya klabu hiyo kuinua na kuthamini soka la wanawake nchini.
“Ni jambo la kujivunia kuona wanawake wakipata nafasi na kuthaminiwa kwa juhudi zao. Tunatarajia haya kuwa ni mwanzo wa safari ya mafanikio zaidi,” alisema Arafat



