Nyumbani

Jeshi Stars: Tutatetea ubingwa msimu ujao

DAR ES SALAAM: KAIMU Meneja wa Jeshi Stars, Charles Malima, amesema timu hiyo haitaridhika na ubingwa ilioutwaa msimu huu, badala yake imeanza maandalizi ya kuhakikisha inautetea katika msimu ujao.

Malima amesema ubingwa huo umetokana na kazi kubwa, nidhamu na kujituma kwa wachezaji waliopambana katika msimu uliokuwa na ushindani mkali.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa pia na sapoti kubwa kutoka kwa uongozi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao umeendelea kuiwezesha timu hiyo katika safari yake ya mafanikio.

Alitoa shukrani za pekee kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa mchango wake katika kuiunga mkono Jeshi Stars hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa.

“Kutwaa ubingwa si mwisho wa safari yetu. Tumeanza kujipanga kuimarisha kikosi ili kuhakikisha tunautetea ubingwa huo msimu ujao,” amesema Malima.

Ameongeza kuwa pamoja na maandalizi ya msimu mpya, Jeshi Stars imeanza kuelekeza nguvu kwenye mashindano yajayo ya Kombe la Mkuu wa Majeshi ‘CDF Cup’ na BAMATA, ikilenga kuendelea kufanya vizuri na kudumisha ubora wake dhidi ya wapinzani mbalimbali.

Related Articles

Back to top button