Simba SC kupasha tena kesho

DAR ES SALAAM: Wekundu wa Msimbazi Simba Sports club wanatarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki kesho inayolenga kukiimarisha kikosi chao kabla ya kukutana na Al Ahly Tripol ya Libya kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba walianza kucheza dhidi ya Al Hilal ya Sudan na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 bao likiwekwa wavuni na straika wao Lionel Ateba, mchezo huo uliopigwa la KMC Complex.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally ameiambia Spotileo, kuwa wanautumia muda huu Ligi ikiwa imesimama kupisha michuano ya Kimataifa kwa Timu za Taifa kuendelea kukinoa kikosi chao kuhakikisha kinafanya vizuri hasa Michuano ya Kombe la Shirikisho.
“Kwa sasa tunaendelea na program yetu ya mazoezi na tutakuwa na mchezo mwingine wa kirafiki Jumamosi. Tumeendelea na program ya mazoezi kwa sababu timu yetu bado inahitaji muda mwingi zaidi kwani wachezaji wengi ni wapya.
“Tutacheza dhidi ya JKT Tanzania Jumamosi (kesho) ikiwa ni maandalizi kuelekea mchezo wetu wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripol ya Libya, wachezaji waliopo wanaendelea kujifua kwenye Uwanja wa mazoezi,” amesema Ahmed.
Akizungumzia hali ya kiafya ya wachezaji wao, Ahmed alisema mpaka sasa timu yao ipo vizuri ikiwa haina majeruhi zaidi ya kipa wao Ayoub Lakred ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiwaambia mashabiki kuendelea kuisapoti timu yao.