Idris Elba kuhamia Afrika miaka mitano hadi 10 ijayo

LONDON: NYOTA wa tamthilia ya ‘Luther’, Idris Elba amefichua kwamba yupo katika maandalizi ya kuondoka nchini Uingereza ili ahamie Afrika katika mpango wake wa kufungua studio za filamu Tanzania visiwani (Zanzibar), Ghana na Sierra Leone.
Elba amezaliwa London nchini uingereza, mama yake anaitwa Eve anatoka nchini Ghana na baba yake Winston anatokea nchini Sierra Leone.
Elba aliiambia BBC: “Nadhani nitahama katika miaka mitano hadi 10 ijayo, Mungu akipenda. Niko hapa ili kuimarisha tasnia ya filamu, huo ni mchakato wa miaka 10, sitaweza kufanya hivyo kutoka ng’ambo. Ninahitaji kuwa ndani ya nchi, barani Afrika.”
Idris aliendelea kufichua kuwa anataka kutenga muda wake akiwa katika mji mkuu wa Ghana, Accra na mji mkuu wa Sierra Leone wa Freetown pamoja na visiwani Zanzibar.
Aliongeza: “Nitaishi Accra, nitaishi Freetown, nitaishi Zanzibar. Nitajaribu kwenda mahali ambapo wanasimulia hadithi, hiyo ni muhimu sana kwangu.”
Idris alisisitiza kwamba anataka kusaidia kubadilisha jinsi Afrika inavyoonekana, akisema: “Ukitazama filamu yoyote au kitu chochote kinachohusiana na Afrika, utakachoona tofauti, jinsi tulivyokuwa watumwa, jinsi tulivyokuwa na ukoloni, lakini ukifika Afrika, utagundua kuwa sio kweli.
“Kwa hivyo, ni muhimu sana tumiliki hadithi za mila zetu na za utamaduni wetu na za lugha zetu zenye utofauti kati ya lugha moja na nyingine. Ulimwengu haujui,
“Lazima tuwekeze katika kusimulia hadithi zetu kwa sababu unaponiona, unaona toleo lako kidogo na hilo hututia moyo.” Alieleza Idris Elba.