Ibenge: Tunahitaji kushinda kila mchezo

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema lengo kuu la timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB ni kushinda kila mchezo ulioko mbele yao na kufuzu hatua zinazofuata licha ya ushindani kuwa mkubwa na muda kuwa mfupi.
Akizungumza baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Endumenti FC jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Ibenge amesema michuano hiyo inahitaji umakini mkubwa na matokeo chanya kila mechi ili kufikia malengo.
Kocha huyo alikiri kuwa kiwango cha jumla cha timu hakikuwa kizuri sana, akieleza kuwa aliwatumia wachezaji wengi ambao hawajapata muda wa kutosha kucheza katika mechi za hivi karibuni, lakini alifurahishwa na nafasi aliyopata ya kuwapima.
Ibenge ameongeza kuwa mchezo huo pia ulikuwa na faida ya kimkakati kwa kikosi chake kwani uliwapa nafasi ya kuwapumzisha baadhi ya nyota wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya michezo ijayo yenye ushindani mkubwa.
Kutokana na ushindi huo, Azam FC imefanikiwa kutinga hatua ya 32 bora ya michuano hiyo huku kocha huyo akieleza kuwa wataendelea kuboresha kiwango cha timu kadri wanavyoendelea na ratiba ya mashindano.




