Kwingineko

Mashabiki Afrika watafurahia UEFA kupitia CANAL+ kuanzia 2027-2031

CANAL+ imetangaza kupata haki za kipekee za kuonesha mashindano yote ya klabu za wanaume ya UEFA katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kupitia makubaliano hayo mapya, kuanzia katikati ya mwaka 2027 hadi mwaka 2031, wateja wa CANAL+ katika zaidi ya nchi 40 za ukanda huo wataweza kufuatilia mechi za UEFA Champions League, UEFA Europa League na UEFA Conference League.

Mashindano hayo yatazikutanisha klabu kubwa kutoka England, Hispania, Italia, Ufaransa, Ujerumani na Ureno, pamoja na nyota mbalimbali wa soka duniani akiwemo Victor Osimhen, Ademola Lookman, Serhou Guirassy, Amad Diallo, Bryan Mbeumo, Antoine Semenyo, Nicolas Jackson, Kylian Mbappé, Ousmane Dembélé, Lamine Yamal, Erling Haaland, Michael Olise, Achraf Hakimi na Harry Kane.

Kwa upande wa nchi zinazozungumza Kiingereza na Kireno barani Afrika, SuperSport itaendelea kuwa jukwaa la matangazo ya mashindano ya klabu za UEFA kupitia haki zake za kipekee katika maeneo husika.

Katika nchi zinazozungumza Kifaransa, makubaliano hayo yatarejesha matangazo ya UEFA Champions League kupitia CANAL+ Sport, huku kwa mara ya kwanza kituo hicho kikitarajiwa pia kuonesha UEFA Europa League na UEFA Conference League kwa haki za kipekee katika lugha ya Kifaransa.

Mbali na mashindano ya UEFA, vituo vya SuperSport na CANAL+ Sport vinaendelea kurusha mashindano mbalimbali ya soka duniani, yakiwemo Betway Premiership, Premier League, LALIGA EA SPORTS, Ligue 1 na TotalEnergies Women’s Africa Cup of Nations Morocco 2026.

Mkurugenzi Mtendaji wa CANAL+, Maxime Saada, amesema kampuni hiyo imepiga hatua kubwa kwa kupata haki hizo za kipekee, akieleza kuwa zitawapa wateja fursa ya kufuatilia mashindano makubwa zaidi ya klabu barani Ulaya kwa misimu minne kuanzia mwaka 2027 hadi 2031.

Amesema hatua hiyo inaendelea kuimarisha nafasi ya CANAL+ kama moja ya majukwaa makubwa ya maudhui ya michezo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku akitoa shukrani kwa UC3 na timu za Relevent kwa kuendelea kuiamini kampuni hiyo kufuatia makubaliano mengine yaliyofikiwa katika nchi za Ufaransa, Uswisi, Ubelgiji, Poland na Austria.

Related Articles

Back to top button