Muziki

Lady Jaydee na Alikiba wafungua ukurasa mpya

DAR ES SALAAM: Baada ya miaka kadhaa ya kuonekana kuwa na tofauti zilizozua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva, msanii Judith Wambura maarufu Lady Jaydee na mwanamuziki Alikiba wameonesha dalili za kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wao wa kikazi na kirafiki.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, wasanii hao wanatarajiwa kushiriki tukio maalumu litakalofanyika wiki hii katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, jambo ambalo limeongeza hisia kuwa tofauti zilizokuwepo huenda zimeanza kuyeyuka.

Tofauti kati ya wasanii hao zilianza kupewa uzito mwaka 2021 baada ya shabiki mmoja kuuliza kupitia mtandao wa X, uliokuwa ukijulikana zamani kama Twitter, ni lini wawili hao wangerejea studio kurekodi wimbo mwingine wa pamoja kufuatia mafanikio ya kolabo yao ya Single Boy.

Akijibu swali hilo wakati huo, Lady Jaydee alisema hakuwa na mpango wa kufanya kazi tena na Alikiba, kauli iliyoibua hisia tofauti kwa mashabiki wengi walioamini kuwa kulikuwa na sintofahamu kati ya mastaa hao wawili wa muziki wa Tanzania.

Mwaka 2025, Alikiba alipokuwa akiadhimisha miaka 20 tangu aanze safari yake katika muziki wa Bongo Fleva, alizungumzia kauli hiyo na kueleza kuwa ilimshangaza kwa sababu hakumbuki kuwahi kumkosea Lady Jaydee kiasi cha kufikia hatua ya kushindwa kushirikiana naye tena.

 

Related Articles

Back to top button