Nyumbani

Kagere, Okwi kuipa mvuto Simba Day 2026

DAR ES SALAAM: IKIWA imebaki siku moja kufanyike tamasha la Simba 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, nyota wa zamani wa klabu hiyo, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wametangaza, kuwa miongoni mwa wageni watakaong’arisha tukio hilo.

Kagere, ambaye aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Simba, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kusherehekea siku hiyo kubwa, akisema Simba Day imekuwa sehemu muhimu ya kuunganisha timu na wapenzi wake.

“Nimekuja Tanzania kwa ajili ya Simba Day. Nawakaribisha mashabiki wote wa Simba, naomba muje kwa wingi kwa sababu itakuwa siku kubwa na mchezo mzuri wa kirafiki. Tushirikiane kuifanya siku yetu iwe ya kukumbukwa,” amesema Kagere.

Mshambuliaji huyo raia wa Rwanda amesema moja ya kumbukumbu kubwa kwake katika Simba Day ni ile ya mwaka 2019 wakati Simba ilipocheza dhidi ya Dynamos ya Zambia, ambapo alifunga hat-trick.

“Mechi hiyo ilikuwa muhimu sana kwangu kwa sababu nilikuwa nimeanza kupata maandalizi mazuri ya mwili. Naweza kusema hapo ndipo mwanzo wa mafanikio ulipoanza, baadaye tukafanikiwa kuchukua ubingwa,” amesema.

Kagere pia alikumbuka namna mashabiki wa Simba walivyomuonesha upendo mkubwa wakati wa moja ya matukio ya Simba Day, akisema sapoti yao ilimpa nguvu hata wakati alipokuwa akikabiliwa na changamoto.

Wakati huohuo, miongoni mwa wageni maalumu watakaokuwa sehemu ya Simba Day 2026 ni Emmanuel Okwi, ambaye ataandaliwa siku maalumu ya kuagwa rasmi kwenye soka kwa heshima anayostahili.

Okwi, ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kuacha alama kubwa katika historia ya Simba, atashiriki pia mchezo wa kirafiki akiwa amevaa jezi ya Simba SC, ikiwa ni sehemu ya kumuaga mbele ya mashabiki wa klabu hiyo.

Ujio wa Okwi unatarajiwa kuongeza mvuto wa Simba Day, kutokana na historia yake na uhusiano mkubwa alioujenga na mashabiki wa Simba wakati akiwa mchezaji wa timu hiyo.

Simba Day 2026 inatarajiwa kuwa jukwaa la kutambulisha mipango ya msimu mpya, wachezaji wapya pamoja na kusherehekea historia ya klabu hiyo sambamba na mashabiki wake.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button