Hamisa Mobetto: Sina Tatizo Mume Wangu Akioa Mke wa Pili

DAR ES SALAAM:MKE wa mchezaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, Hamisa Mobetto, amesema hana tatizo iwapo mume wake ataamua kuoa mke wa pili.
Hamisa alisema kuwa, kwa kuwa dini ya Uislamu inaruhusu ndoa za wake wengi, na yeye hana pingamizi ikiwa mume wake ataona hitaji la kuongeza mke mwingine.
“Maadamu mimi ni mke wa kwanza, ikiwa mume wangu anahisi hitaji la kuoa mke mwingine, nitakuwa tayari. Sina shida nayo,” alisema Hamisa katika mahojiano ya hivi karibuni.
Katika Uislamu, mwanamume anaruhusiwa kuwa na wake hadi wanne, mradi tu anawatendea kwa usawa katika masuala ya kifedha, mipango ya maisha, na majukumu mengine chini ya uangalizi wake.
Hamisa, ambaye ni mama wa watoto wawili, awali alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na staa wa Bongo Flava, Diamond Platnumz, wakati Diamond alikuwa katika uhusiano na mfanyabiashara kutoka Uganda na Afrika Kusini, Zari Hassan.
Uhusiano huo ulizaa mtoto wa kiume, na wakati huo Hamisa alifichua kuwa alikuwa mjamzito wa Diamond, hali iliyozua sintofahamu kubwa. Wengi walihisi kuwa hilo lilichangia kuachana kwa Diamond na Zari, ingawa Diamond aliwahi kukanusha madai hayo katika juhudi za kuokoa uhusiano wake na Zari.
Hamisa pia alifichua kuwa aliwahi kutarajia Diamond angemuoa kutokana na uhusiano wao wa muda mrefu kabla ya Diamond kujihusisha na wanawake wengine, akiwemo Zari.
Alisema alikuwa tayari kuwa mmoja wa wake wa Diamond katika ndoa halali. Hata hivyo, alipohamia kwenye uhusiano na Aziz Ki, alishikilia msimamo wake huo huo kuhusu ndoa hadi alipofunga ndoa rasmi.