Tausi Likokola kurudi tena kwa jamii
MWANAMITINDO mstaafu wa kimataifa, Tausi Likokola amesema anaandaa ‘documentary’ ambayo sehemu ya mapato yake atarudisha kwa jamii.
Likokola amesema kipindi cha nyuma alianza kupeleka kahawa ya Tanzania nchini Marekani na kupitia hilo alisaidia baadhi ya wakulima hata hivyo amesema ataendelea kusaidia kwa atakavyoweza.
Akizungumza na SpotiLEO, Likokola amesema katika kuendelea na jitihada za kusaidia jamii wakiwemo wasichana, anapanga kuirudisha taasisi yake nchini.
“Tausi Aids Fund nilianzisha Ujerumani na ilifanikiwa kufanya kazi na foundation za Tanzania kama Wamata kipindi cha nyuma na kutoa michango. Pia nilifanya Dar es Salaam. Baada ya kuhama Ujerumani niliendelea kusaidia wenye ualbino kwenye shule za wasichana na hata nilitengeneza ‘Tv show’ kuelimisha,” amesema Likokola.
Amesema katika jitihada zake za kuisaidia jamii amekuwa akiungwa mkono na Serikali hali inayofanya aendelee kuisaidia jamii na kuweka nguvu zaidi katika eneo hilo.
“Miaka ya nyuma hata mabalozi wetu Ujerumani na Marekani walinishika mkono sana juhudi zangu, na kila nilipokuwa narudi Tanzania, pia serikali walinitambua na kunipa sapoti,” amesema Likokola.
Amesema ameanza tena kushughulika na mambo machache na kwamba kupitia atakayofanya ana imani ya kuungwa mkono na serikali.