Mitindo

Tausi Likokola: Tuige walioendelea kupata wanamitindo bora

MWANAMITINDO mstaafu wa kimataifa, Tausi Likokola ameshauri ili Tanzania itoe wanamitindo wengi bora wahusika wanapaswa kuiga michakato na vigezo vya mataifa yaliyoendelea kwenye tasnia hiyo.

Akizungumza na SpotiLEO, Likokola ambaye pia ni mwandishi wa vitabu amesema mashindano ya urembo yalikuwa njia ya warembo kuingia kwenye fasheni bahati mbaya vigezo vinatofautiana.

Amesema wapo warembo waliokuwa na vigezo walifanikiwa na wengine walishindwa kutokana na kutokuwa na vigezo.

Hata hivyo Likokola ameshauri kuwa ni muhimu wasichana wanaotamani kuingia kwenye fasheni ni vyema wazazi pia wakahusika kuhakikisha watoto wao wanakutana na watu sahihi katika fasheni.

“Ni muhimu msichana akiwa anaelekea kwenye fasheni, shule aendelee na wazazi wajihusishe kuhakikisha anakutana na watu sahihi wanaojua cha kufanya na kwenda na ‘portfolio’ yake,” amesema Likokola.

Akizungumzia uthubutu wa wasichana kwenye eneo hilo, Likokola amesema kipindi cha nyuma alipokuwa akifanya programu kwenye televisheni aligundua wasichana wengi wanahitaji kuingia kwenye fasheni ila kuna changamoto katika njia za kufanikisha hilo.

Amesema fasheni nje ya Tanzania ni mfumo wa ajira, kuna wakala wanaowakilisha na wote wanashirikiana na kulipana vizuri.

“Wote wanashirikana na kampuni kwa matangazo, maonesho, magazeti na wanalipana vizuri, ni kazi inayoheshimika na siyo kupoteza muda,” amesema Likokola.

Related Articles

Back to top button