Nyumbani

Baba Samatta: Matusi yamemkimbiza Mbwana Samatta Timu ya Taifa

DAR ES SALAAM: BABA wa Nahodha wa timu ya Taifa Stars Mbwana Samatta, Ally Samatta amesema mwanae amepumzika kuchezea timu ya taifa kwa sababu ya matusi na lugha mbaya anazopata kutoka kwa mashabiki pindi anapokuwa akiitumikia timu ya taifa.

Mzee Samatta aliongea hayo katika kipindi cha michezo cha redio moja ya jijini Dar es Salaam alipohojiwa kuhusu mwanae na sababu za kupumzika kucheza katika timu ya taifa huku akiwa anahitajika kutokana na uzoefu wake wa kucheza soka kimataifa.

Mzee Samatta amesema sababu kubwa ya Mbwana Samatta anayechezea timu ya PAOK ya nchini Ugiriki kuomba kupumzika timu ya taifa kunatokana na kuandamwa na simu pamoja na meseji za matusi na tuhuma za kwamba hachezi vizuri akiwa na timu ya taifa lakini akiwa ulaya anacheza vizuri.

“Ndiyo Samatta ameandika barua TFF na TFF wanajua sababu za mwanangu kutotaka kucheza timu ya taifa amewaandikia barua amewaambia kwamba anatukanwa sana anapocheza timu ya taifa, amekuwa akipokea meseji nyingi za matusi hivyo ametaka kupumzika kwa muda usiojulikana lakini TFF wamelikataa ombi lake hilo,” amesema Mzee Samatta.

Ally Samatta ameongeza kwamba mwanae hakumshirikisha katika uandikaji wa barua hiyo lakini kupitia meneja wake anafahamu kwamba amepeleka barua TFF na changamoto zake hizo amezieleza kwa viongozi wa mpira nchini lakini wamekataa ombi lake la kustaafu soka.

“Hakunishirikisha anajua jibu langu lingekuwa hapana nisingemkubalia aiache taifa stars naamini nchi bado inahitaji mchango wake ila kwasababu hakunishirikisha wala sitamuuliza maana anaweza kunikana umesikia wapi kama nimeandika barua nitabaki sina jibu lakini akinishirikisha jibu langu ni hapana maana taifa bado linamuhitaji na bado anaweza kuisaidia taifa stars,” amesema Mzee Ally Samatta.

Mzee huyo ameongeza kwamba kabla ya mashabiki na baadhi ya watu wanaowafahamu walikuwa wakimpigia simu yeye wakimsema kwa nini mwanae achezi vizuri timu ya taifa naye aliwakataza watu hao waache kumpigia simu hizo kwa kuwa yeye si mchezaji kwa sasa wamfuate Mbwana mwenyewe.

“Walikuwa wananipigia simu nyingi na meseji za ajabu ajabu wananisema kuhusu mwanangu kwamba achezi vizuri niliwakataza kwa kuwafokea sitaki wanipigie simu tena mimi si mchezaji anayecheza ni mwanangu hivyo wampigie yeye atawajibu, nashukuru waliacha kunipigia na kunisumbua kuhusu mwanangu,” ameeleza Mzee Samatta.

Mbwana Ally Samatta amezaliwa 23 Disemba 1992 ni mchezaji wa mpira wa miguu wa Tanzania katika klabu ya PAOK Thessaloniki FC ya nchini Ugiriki aliwahi kucheza Feberbahce ya nchini Uturuki, akacheza Aston Villa ya nchini Uingereza.

Samatta alianza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya African Lyon mwaka 2008 nchini Tanzania. Alisajiliwa na klabu ya Simba S.C. mwaka 2010, ambapo alicheza katika nusu msimu tu kabla ya kujiunga na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Alicheza kwa miaka mitano ndani ya TP Mazembe na kujijengea nafasi katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo.

Mwaka 2015, alishinda taji la mchezaji bora wa mwaka wa Afrika, na kumaliza msimu akiwa mfungaji bora wa mashindano ya klabu bingwa Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika) na kuisaidia klabu yake kushinda taji hilo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button