Guardiola: Rodri asiharakie uwanjani

LONDON: Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amemshauri staa wa timu hiyo Rodrigo Cascante Hernández maarufu Rodri kutojisukuma sana kuwahi uwanjani na badala yake atumie muda huu kujiimarisha zaidi.
Guardiola amesema licha ya nyota huyo kuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chake anatamani arejee akiwa kamili ili aepuke kukaa tena kwenye majeraha kwa muda mrefu
Rodri, raia wa Hispania na mshindi wa tuzo ya Balon D’or alipata majeraha katika mchezo ligi kuu dhidi ya Arsenal mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2 mwezi Septemba.
Mchezaji huyo alisafiri na kikosi kuelekea Paris kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya PSG mapema mwezi huu, na tangu mda huo amekuwa akionekana kwenye mechi na mazoezi ya Manchester City jambo lililozua tetesi kuwa huenda akawa sehemu ya kikosi hicho kitakachocheza hatua ya 16 bora ya UCL.
“Yuko vizuri japo siwezi kuthibitisha hilo jeraha ni jeraha siku zote naamini kwenye majeraha ni muhimu sana kuheshimu muda, ni vyema kuwa nae tena uwanjani, mazoezini na sehemu nyingine lakini natamani atulie, kitu muhimu sana kwake ni kupona” amesema Pep
Baada ya upasuaji wa Rodri jijini Madrid taarifa zilieleza anahitaji muda mrefu zaidi kupona ikikadiriwa huenda asicheze kabisa msimu huu lakini kasi ya kupona kwake iliibua taarifa nyingine za huenda akarejea kabla ya muda uliotegemewa.