Gigy Money: Maisha yamenifundisha mtu anaweza kubadilika

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Gift Stanford ‘Gigy Money’, amesema maisha yamemfundisha kuwa mtu anaweza kubadilika na kuwa bora zaidi pale anapopata mwongozo sahihi katika maisha.
Kupitia ujumbe aliyouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, msanii huyo amesema anatambua kuwa zamani hakuwa kama alivyo sasa, kwani alipitia changamoto na kufanya makosa mbalimbali yaliyomjengea uzoefu wa maisha.
“Maisha yamenifundisha kitu kikubwa sana… mtu anaweza kubadilika. Mimi mwenyewe najua sikuwa hivi nilivyo leo. Nilikuwa na mapungufu yangu, makosa yangu na njia zangu ambazo pengine hazikuwa sahihi. Lakini Mungu ni mkubwa. Anapogusa moyo wa mtu, kila kitu kinaweza kubadilika,” ameandika.
Msanii huyo ameeleza kuwa mabadiliko yake yametokana na rehema na uongozi wa Mungu, akisisitiza kuwa mafanikio na hatua alizofikia sasa si kwa nguvu zake binafsi bali kwa neema ya Mungu
Aidha, Gigy Money alizungumzia suala la ndoa akisema kuwa ndoa si kitu kinachowapata watu wote kirahisi, bali ni baraka maalum inayohitaji kuthaminiwa na kulindwa.
“Nataka kusema kitu kwa unyenyekevu kabisa, ndoa si riziki anayopata kila mtu. Ni baraka maalum. Namshukuru Mungu kwa kunibariki na zawadi hii. Nitajitahidi kuitunza, kuheshimu ndoa yangu, kumheshimu mume wangu na kuilinda familia yangu kwa nguvu zote,” ameeleza.
Katika ujumbe wake, msanii huyo aliwatia moyo watu wanaopitia changamoto mbalimbali maishani wasikate tamaa, akisisitiza kuwa mabadiliko yanawezekana pale mtu anapomtegemea Mungu.
“Kwa yeyote anayepitia changamoto au anayejiona hawezi kubadilika, tambua tu Mungu bado yupo nyuma ya pazia la maisha yako. Akiamua kukuinua, hakuna anayeweza kuzuia,” amehitimisha.




