Geita Gold yapiga hesabu kurudi Ligi Kuu

KLABU ya Geita Gold FC imesema kwa uwekezaji iliofanya msimu huu wana kila sababu ya kupambana na kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu hiyo iliyoshuka msimu uliopita imedhamiria kutokaa muda mrefu kwenye Championship ikisema imejipanga vizuri kupambana na kutimiza malengo yao ya kurejea.
Akizungumza na SpotiLeo Ofisa Habari wa Geita Gold Samwel Dida amesema “tumekuja kujipanga upya kutengeneza mfumo mpya wa utawala. Tunarudi vizuri bado mapema tumecheza michezo minne, malengo yetu lazima tuyakamilishe,”
Geita ilikuwa ugenini kwa michezo mitatu na kati ya hiyo, imeshinda miwili na sare moja. Ilishinda 3-0 dhidi ya Transit Camp, 1-0 dhidi ya Kiluvya na sare tasa dhidi ya Mbuni.
“Tumeanza vizuri ligi katika michezo minne, tumeshinda michezo miwili na kupata sare mbili, huu ni mwanzo mzuri kwetu bado kuna safari ndefu na tunaamini tutaitimiza,”amesema.
Amesema wanarejea kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Nyankumbu kucheza michezo mitatu ijayo na migumu dhidi ya African Sports, Mtibwa Sugar na Polisi Tanzania.
“Tunahitaji jitihada kubwa ili kuwa bora zaidi, tunaamini watarekebisha baadhi ya maeneo yanayohitaji kuwekewa nguvu. Tuombe mashabiki wazidi kutuombea tuendelee kufanya vizuri na kurejea kunako ligi kuu,”amesema.