Vitisho vyatamalaki kuelekea Dar Boxing Debi

DAR ES SALAAM: MABONDIA mbalimbali wa ngumi za kulipwa nchini wameanza kurushiana vitisho na kutamba ushindi kuelekea tamasha kubwa la Ngumi maarufu kama Dar Boxing Debi litakalofanyika Julai 24, 2026 Dar es Salaam, huku wengi wakiahidi kuwamaliza wapinzani wao kwa njia ya KO.
Tamasha hilo linaloratibiwa na Peak Time Media linatajwa kuwa moja ya matukio makubwa ya ngumi nchini mwaka huu, likiwakutanisha mabondia wenye majina makubwa kutoka ndani na nje ya Dar es Salaam.
Miongoni mwa mabondia wanaovuta hisia za mashabiki ni Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ ambaye amesema yupo katika kiwango bora na amejipanga kufikisha KO yake ya 35 katika maisha yake ya ngumi za kulipwa.
Mbabe amesema tayari amewashinda kwa KO mabondia 34 na anaamini mpinzani wake wa Julai 24 atakuwa wa 35 kuonja kipigo hicho.
“Nataka mashabiki washuhudie ngumi za kweli. Mpinzani wangu ajiandae kwa sababu nina uhakika nitafikisha KO ya 35,” amesema Mbabe huku akisisitiza kuwa hana mpango wa kufanya mzaha ulingoni.
Bondia huyo aliwataja baadhi ya mabondia wakubwa aliowahi kukutana nao akiwemo Francis Cheka, Oswald Morris na Mada Maugo, akisema uzoefu wake unampa nguvu ya kuingia kwenye pambano hilo kwa kujiamini zaidi.
Naye Juma Choki amethibitisha kurejea ulingoni baada ya kutokuwepo kwa muda mrefu, akiahidi kutoa burudani ya hali ya juu kwa mashabiki wa ngumi za kulipwa.
Choki, ambaye hivi karibuni alimshinda kaka yake Nasib Ramadhan, amesema mpinzani wake anapaswa kufanya maandalizi ya kweli kwa sababu analenga kurejea kwa kishindo.
Kwa upande wake, Hussein Itaba amesema: “Bondia anatakiwa kuonesha vitendo kuliko maneno. Mpinzani wangu afanye mazoezi apunguze kuongea,” amesema Itaba.
Katika upande wa wanawake, bondia mahiri Sarah Alex baada ya kushindwa kwake dhidi ya Halima Vunjabei kumempa somo kubwa na kumjenga na sasa amesema amejipanga kurejea akiwa imara zaidi na ana ndoto ya kulipa kisasi kwa mabondia wote waliowahi kumshinda.
Wengine watakaopanda ni Haidari Mchanjo, Issa Molel maarufu kwa jina la ‘Masai’, Oscar Richard, Dorisia Mazige na Dorothea Muhoza.




