Filamu kuhimiza utalii wa ndani

DAR ES SALAAM: WASANII nchini wametakiwa kutumia filamu na makala kuhamasisha utalii wa ndani kwa kutangaza vivutio vya Tanzania, kama ilivyofanywa na onesho maalumu la Guardians of The Peak Season I linaloangazia safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza katika uzinduzi wa kuelekea msimu wa pili wa makala hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Filamu, Emmanuel Ndumukwa amesema onesho hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya filamu, utalii, mazingira pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Amesema lengo la mradi huo ni kujenga hamasa kwa vijana na wanafunzi kushiriki katika hatua mbalimbali za utayarishaji wa filamu na makala, huku wakipata nafasi ya kujifunza kuhusu fursa zilizopo katika sekta za filamu, utalii na utunzaji wa mazingira.
“Bodi ya Filamu Tanzania inaunga mkono jitihada zinazofanywa na mradi wa Guardians of The Peak katika kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kushiriki na kujifunza zaidi kuhusu tasnia ya filamu na mchango wake katika maendeleo ya taifa,” amesema Ndumukwa.
Ameongeza kuwa bodi hiyo ipo tayari kushirikiana na wanafunzi katika kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali ya kifilamu itakayosaidia kuhamasisha utalii pamoja na utunzaji wa mazingira nchini.
Kwa mujibu wa waandaaji, Guardians of The Peak Season I imekuwa chachu ya kuhamasisha vijana kuhusu maisha, ndoto na mapambano ya kufikia mafanikio kupitia mshikamano, ujasiri, kujituma na utunzaji wa mazingira.
Naye Mkurugenzi wa Guardians of The Peak, muandaaji wa Filamu hiyo Ram Ally amesema msimu wa kwanza uliwakutanisha washiriki kutoka mazingira tofauti, kila mmoja akiwa na historia, changamoto na ndoto zake binafsi.
Baadhi yao walitoka katika familia za kawaida huku wengine wakikabiliana na mazingira magumu ya maisha, lakini wote walikutana katika safari ya kutafuta mabadiliko kupitia kupanda Mount Kilimanjaro.
Ram amesema kupitia safari hiyo, washiriki walijifunza kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu, nidhamu na moyo wa kutokata tamaa.
“Lengo kubwa la Guardians of The Peak Season I halikuwa tu kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro, bali kuonyesha kuwa kila kijana ana uwezo wa kushinda vikwazo vinavyomzunguka,” amesema.
Ameeleza kuwa kipindi hicho pia kinaonyesha umuhimu wa mshikamano, kusaidiana na kujenga urafiki unaovuka mipaka ya mashindano.
Katika uzinduzi huo, wageni waalikwa walipata fursa ya kutazama filamu fupi ya Guardians of The Peak Season I iliyobeba ujumbe kuwa safari ya kupanda mlima ni sawa na safari ya kujitambua, huku kila hatua ikisisitiza umuhimu wa kuamini ndoto na kupambana ili kuzitimiza.
Mwisho wa msimu huo, washiriki walifanikiwa kufikia hatua muhimu katika safari yao, jambo lililoonyesha kuwa ushindi wa kweli haupo tu katika kufika kileleni, bali katika mabadiliko ya ndani anayopitia mtu.
Makala hiyo imeelezwa kuwa zaidi ya burudani, kwani imeendelea kuwa jukwaa la kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu umuhimu wa juhudi, mshikamano na imani katika kutimiza ndoto zao.



