BurudaniFilamu

ACCEPTED

KWA kifupi wanamwita B lakini jina lake kamili ni Bartleby Gaines. Ni kijana ambaye amemaliza kidato cha nne lakini amekosa alama za kumwezesha kujiunga na masomo ya
chuo.

Licha ya kujaribu kutuma maombi kwenye vyuo mbalimbali lakini hakubaliki kutokana na alama zake kuwa za chini. Wakati huo nyumbani kwao kunafukuta kwa kuwa baba, mama na dada yake mdogo ‘wanamkomalia’ kwamba lazima apate chuo kwa sababu mtaani hakufai.

Wasilolijua ni kwamba hakuna hata chuo kimoja kilichomkubali na sasa anashindwa
kuwaeleza wazazi wake ukweli. Baada ya maneno kuwa mengi nyumbani anajiongeza,
anafikiria ‘nje ya boksi’ na kuwafuata ‘washkaji’ zake ambao wao pia wamekosa alama za kuwapeleka chuo, na anawashirikisha kuhusu mpango wake.

Mpango huo unahusisha kutengeneza tovuti ya uongo ya chuo ambacho hakipo na kisha wajitumie barua nyumbani kwamba wamechaguliwa kujiunga na chuo hicho. Wanaamini kwa kufanya hivyo wazazi wao watawapa fedha zitakazowawezesha kufanya mambo mengine.

Bartleby anamfuata rafiki yake Sherman Schrader III ambaye amekubaliwa kusoma katika Chuo cha Harmon na kumwomba amsaidie kutengeneza tovuti ya chuo kinachoitwa South
Harmon Institute of Technology (SHIT) na kisha barua zinatumwa nyumbani.

Wazazi wanafurahi na kuwapa fedha vijana hao wakiamini kuwa wamepata chuo. Sasa ishu inakuwa, itakuwaje endapo wazazi watataka kuwasindikiza vijana wao chuoni ili wakione
chuo ambacho watoto wao wanasoma?

Bartleby na wenzake wanaamua kukodisha jumba la zamani ambalo sasa halitumiki ambalo mwanzoni lilitumika kama hospitali ya wagonjwa wa akili, wanalikarabati na linakuwa na
mwonekano wa chuo na wanaweka bango juu lenye maandishi “South Harmon Institute of Technology (SHIT)”.

Kisha wanamuandaa Ben Lewis, mjomba wa Sherman ambaye aliwahi kuwa profesa wa chuo kimoja ili ajifanye mkuu wa chuo na kukutana na wazazi wa wanafunzi. Sasa kila kitu kinakaa sawa.

Hata hivyo, mpango wao ‘unabuma’ baada ya kusahau kuifunga tovuti ya chuo hicho waliyoitengeneza, kwenye tovuti kuna kitufe ambacho kinamkubali kila mtu anayeomba kwa kubonyeza 1.

Wakati wakiwa wenyewe tu na mwalimu wao ghafla linatokea kundi la vijana takribani 1,000 wanaofika hapo kujiunga baada ya kukubaliwa na kulipia fedha kwenye akaunti ya chuo hicho bandia.

Sasa Bartleby na rafiki zake wanapagawa kwa kuwa ni wao tu wanaojua kuwa chuo hicho ni cha uongo, wanapanga kuwafukuza na wanaitisha kikao lakini kabla Bartleby hajazungumza, kijana mmoja anainuka na kushukuru kwa kuchaguliwa katika chuo hicho kwa kuwa kwa mara ya kwanza sasa ameonekana mtu wa maana nyumbani kwao baada ya
kuishi kwa masimango.

Jambo hilo linamfanya Bartleby kuumia sana hasa anapogundua kuwa vijana hao hawana pa kwenda na hivyo kusitisha mpango wa kuwafukuza huku wakiwa karibisha chuoni na kuwaacha waamini kuwa hicho ni chuo halali.

Lakini tatizo bado lipo palepale, SHIT si chuo halali na wala hawakuwa na mpango wa kukifanya kuwa chuo bali ilikuwa kupata suluhisho la muda kwa yale yaliyokuwa yanatokea nyumbani kwao.

Sasa Bartleby anafikiria nje ya boksi na kumwita kila mtu akimuuliza angependa kusoma nini. Kila mmoja anataja kitu anachokipenda, wapo wanaopenda kupika, kuchonga vinyago, michezo, kuogelea, baiskeli, kuimba n.k.

Kwa kutumia fedha walizolipa, Bartleby ananunua kila kitu kinachotakiwa kwa mafunzo hayo kama mabwawa ya kuogelea, majiko, vifaa vya sanaa n.k. na kila mmoja anapewa nafasi ya kufanya kitu apendacho kwa muda wake na hakuna mwalimu.

Tatizo jingine linaibuka baada ya kutokea mtafaruku kati ya chuo bandia cha South Harmon na chuo halali cha Harmon, na hivyo siri inavuja na kusababisha wazazi wote kuitwa na chuo kinafungwa.

Bartleby anaitwa katika mamlaka ya elimu ili kujieleza kwa nini anaendesha chuo ambacho hakijasajiliwa, siku ya hukumu wanafunzi wote wa chuo hicho bandia wanafika ili kusikiliza hukumu.

Katika utetezi wake, Bartleby anatoa maelezo yanayowafanya jopo la majaji kutafakari upya… Huu unakuwa ushindi mkubwa kwa vijana wenye ndoto chanya. Natumaini umeshawahi kutazama filamu halafu ukajiuliza mwandishi aliwaza kitu gani kabla ya kuandika au mwongozaji aliwaza nini kutengeneza filamu ya aina hiyo.

Hii ni filamu nzuri sana yenye kutia moyo hasa kama wewe ni mmoja wa watu waliofeli kidato cha nne kwa kukosa alama zinazokuwezesha kujiunga na masomo ya kidato cha tano au chuo, na nyumbani ulisemwa sana ukionekana mmoja wa wale wasiostahili kuishi katika hii dunia.

Ni filamu ya dakika 92 iliyojaa ucheshi, ilitoka mwaka 2006 nchini Marekani ikiwa imeandikwa na Adam Cooper, Bill Collage na Mark Perez na kuongozwa na Steve Pink.
Filamu hii ilitengenezwa kwa gharama ya dola milioni 23 na imefanikiwa kuingiza
dola milioni 38.6 kupitia maonesho ya sinema.

Sms: 0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

 

Related Articles

Back to top button