Europa

Euro 2024 ilinoga

MICHUANO ya Mataifa ya Ulaya mwaka 2024  (Euro 2024) iliyofanyika nchini Ujerumani ilikuwa ya kusisimua, ikijaa ushindani mkubwa na burudani ya hali ya juu. Mashabiki walishuhudia vipaji vipya vikichanua, nyota wakubwa wakiangaza, na Hispania ikitwaa taji lao la nne katika historia.

Hatua ya Makundi: Michuano ilianza kwa hatua ya makundi yenye changamoto na ushindani mkubwa.

Hispania iliongoza Kundi B kwa kushinda mechi zote dhidi ya Italia, Croatia, na Albania. Ujerumani iliongoza Kundi A kwa kuonesha ubora wake kama wenyeji wa mashindano,ikishinda michezo miwili na kutoa sare mchezo mmoja. Ureno ilimaliza kileleni mwa Kundi F kwa ushindi wa mechi mbili kati ya tatu. Austria ilishangaza kwa kuongoza Kundi D mbele ya vigogo kama Ufaransa na Uholanzi.

Hatua ya 16 Bora: Hatua ya mtoano ilileta mshangao mwingi hususani kwa timu kama Italia ambaye alikuwa bingwa mtetezi.Timu hiyo iliushangaza ulimwengu kwa kutolewa na Switzerland kwa mabao 2-0. Ujerumani iliwashinda Denmark 2-0 huku Hispania ikiitandika Georgia 4-1 mabapo vijana wake waliendelea kung’ara.Ufaransa ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ubelgiji.Uholanzi iliiondoa Romania kwa mabao 3-0, na Uturuki iliitandika Austria 2-1.Ureno na England zilisonga mbele kupitia penati baada ya suluhu za mechi zao.

Robo Fainali: Wenyeji walipata kibarua kigumu baada ya kushindwa kutamba dhidi ya Hispania na kupigwa 2-1, mabao ya  vijana walioingia kutoka benchi,Mikel Merino na Dani Olmo huku Florian Wirtz naye akitokea benchi na kuifungia ujerumani bao hilo 1. Ureno kwa mara nyingine ilitoa suluhu ya 0-0 na ufaransa na kisha ikatolewa kwa mikwaju ya penati 3-5. Bukayo saka aliisawazishia England na kufanya matokeo yawe 1-1 dhidi ya Uturuki,nao wakaenda hatua ya penati kisha England ikashinda kwa mikwaju 5-3. uholanzi iliiondoa Uturuki baada ya ushindi wa mabao 2-1.

Nusu Fainali: Nusu fainali ya kwanza iliwakutanisha Hispania na Ufaransa, Hispania ilishinda 2-1, Lamine Yamal akiwa bado ana miaka 16 tu aliwaka sana katika mchezo huo akifunga bao safi mbele ya beki mwenye uzoefu mkubwa Theo Hernandez na kisha Dani Olmo akazidi kujitengenezea mazingira ya kuchukua kiatu cha dhahabu kwa kupachika bao la 2. bao la Ufaransa lilifungwa na Kolo Muani. Nusu fainali ya pili ilikuwa kati ya Uholanzi na England ambapo Uholanzi ilianza kupata bao dakika ya 7 kupitia staa wa Leipzig Xavi Simons lakini Harry Kane alirudisha bao hilo dakika 9 baadae baada ya kusababisha penati ambayo aliipiga yeye mwenyewe. Wengi walidhani mchezo ungeenda dakika 30 za nyongeza lakini ‘super sub’ Ollie Watkins aliipa bao la ushindi England katika dakika za jioni kabisa.

Fainali:Kama kawaida fainali ilikuwa ya kusisimua, Hispania dhidi ya England katika dimba la Olympiastadion Berlin ambapo Hispania iliutawala mchezo huo katika kila idara na kufanikiwa kushinda kwa mabao 2-1. Hispania ilipata mabao kupitia Nico Wiliams, dakika ya 47 kwa usaidizi wa Lamine Yamal ambaye siku moja tu nyuma alitoka kutimiza miaka 17. Cole Palmer ambaye alikuwa hapangwi na kocha Gareth southgate kwenye mashindano hayo aliisawazishia England dakika ya 73 lakini kama kawaida ya Hispania, ‘Super sub’ anayeitwa Mikel Oyarzbal alifunga bao dakika ya 86 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa  Marc Cucurella ambaye walipigiana ‘One-two’.Na hivyo, baada ya miaka 12 Hispania akawa bingwa wa Euro 2024, hii ikiwa ni mara ya 4 baada ya 1964, 2008, na 2012.

Nyota wa Michuano: Kiungo mkabaji wa Hispania Rodrigo Hernandez Cascante maarufu kama Rodri alibeba tuzo ya mchezaji bora wa michuano. Tuzo ya mchezaji bora kijana ilienda kwa Lamine Yamal baada ya kufunga bao 1 na kutoa pasi 4 za mabao. Wachezaji 6 walifungamana katika kuwania kiatu cha mfungaji bora wote wakiwa na mabao matatu; Cody Gapko,Harry Kane,Georges Mikautazde,Ivan Schranz, Jamal Musiala na Dani Olmo. Golikipa wa Georgia, Giorgi Mamardashvli alikuwa golikipa bora wa michuano kutokana na kuokoa mpira mara nyingi zaidi, aliokoa mara 29. Goli la Lamine Yamal dhidi ya Ufaransa ilitajwa kuwa goli bora la michuano hiyo.

Euro 2024 ilithibitisha uzuri wa soka la Ulaya, ikileta mshikamano na historia ya kipekee kwa mashabiki wa soka duniani kote.Makala ya 18 ya michuano ya Euro itakuwa na wenyeji wanne ambao ni England,Republic of Ireland,Scotland na Wales na inategemewa kufanyika kuanzia Juni 9 hadi Julai 9 2028.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button