Emerson Foundation yapongezwa kwa kukuza sanaa Zanziba

MKURUGENZI WA Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF), Joseph Mwale ameupongeza Mfuko wa Wakfu wa Taasisi ya Emerson Zanzibar (Emerson’s Zanzibar Foundation) kwa kukuza sekta ya Sanaa Visiwani humo ikiwemo kuibua na kuviendeleza vipaji vya Vijana.
Joseph Mwale amesema hayo katika hafla maalum ya kumpongeza Mohammed Suleiman “Sule” aliyeshinda tuzo ya filamu Bora za Zanzibar zinazotolewa na mfuko huo kila mwaka.
Mshindi huyo ambaye ni Rais wa Chama cha Wasanii Zanzibar alishinda tuzo hiyo kupitia filamu yake ya ‘Uhuru Wangu’ katika tuzo za ZIFF zilizotolewa Agosti 4.
Mwale ameupongeza mfuko huo wa Emerson kwa kuanzisha Tuzo ya Uandishi wa Miswada ya Tamthilia zitakazoshindaniwa kwa mwaka 2025 kwani zitaleta chachu kwa wasanii wa Zanzibar katika ukuaji wao kwenye upande huo muhimu ambao ni Msingi Kwenye masuala ya Uigizaji.
Aidha, Joseph Mwale alisema Emerson’s Zanzibar Foundation imekuwa msaada mkubwa kwa ZIFF kwa kuweza kuhamasisha vijana ambao filamu zao pia zinaoneshwa kwenye Jukwaa hilo kubwa na la Kimataifa la Filamu.
“Emerson’s Zanzibar Foundation mnatusaidia hasa katika hatua yenu hii ya tuzo za Uandishi wa Miswada ya Tamthilia. Vijana wanaenda kupata ajira lakini pia itaibua kazi nyingi upande huu. ZIFF milango ipo wazi kuendelea kushirikiana kufikia ndoto ya kila msanii katika sekta ya filamu Zanzibar.” Amesema Joseph Mwale.
Aidha, viongozi wa Emerson’s Zanzibar Foundation wametangaza rasmi
tuzo hizo za Uandishi wa Miswada ya Tamthilia 2025 ambapo milango ipo wazi kwa watu wote wa Zanzibar.
“Enzi Mpya kwa Uandishi wa Hadithi za Televisheni Zanzibar. Mradi huu maalum umebuniwa ili kuinua sanaa ya uandishi wa miswada ya Tamthilia Zanzibar.
Tuzo hii ya kipekee inalenga kukuza na kutambua vipaji bora vya ndani ya nchi katika uandishi wa miswada, kwa lengo la kuandaa miswada yenye ubora wa hali ya juu inayofaa kwa uzalishaji wa televisheni.
Katika miaka ya hivi karibuni, tasnia ya filamu ya Tanzania imeona mabadiliko makubwa kutoka kwenye filamu ndefu na fupi kuelekea kwenye Tamthilia za televisheni, ambapo watayarishaji na waongozaji wameanza kutambua faida za muundo huu.