TWIGA STARS lengo lake ni kutetea Kombe la Cosafa

TWIGA Stars mwaka jana ilialikwa kwenye Mashindano ya Cosafa na kufanikiwa kubadili rekodi ya timu ya Taifa ya Afrika Kusini waliokuwa mabingwa wa mashindano hayo kwa mara saba mfululizo.
Kwa sababu ndio mabingwa watetezi, mwaka huu pia wamealikwa tena katika mashindano hayo, ambayo yanaanza kutimua vumbi Jumanne Agosti 31 na kumalizika Septemba 11, Port Elizabeth, Afrika Kusini.
Twiga Stars ilifuta makosa ya kuishia hatua ya makundi 2019 ikasema inakwenda kuhakikisha makosa yote ya huko nyuma wanayafanyia kazi, lengo lao kubwa zaidi likiwa ni kubeba kombe na kurudi nalo nyumbani Tanzania.
MSIMU ULIOPITA
Twiga Stars walitawazwa mabingwa baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Malawi na kuhitimisha mashindano bila kufungwa.
Katika hatua ya nusu fainali waliifunga Zambia kwa penalti 4-2 baada ya kumaliza muda wa mchezo kwa sare ya 1-1. Katika hatua ya makundi Twiga Stars ilizichabanga Botswana 2-0, Sudan Kusini 3-0 na Zimbabwe 2-0 na kuacha historia ya kipekee katika Ukanda wa Kusini.
WACHEZAJI BORA
Kwa namna ambavyo Twiga Stars ilionesha makeke yake ilifanikiwa kutoa mchezaji bora kwenye kila mechi na mchezaji bora wa mashindano. Nahodha Amina Bilali aliibuka mchezaji bora wa mashindano hayo, pia mchezaji bora wa mchezo wa nusu fainali.
Mwanahamisi Omar alikuwa mchezaji bora wa mchezo dhidi ya Botswana, Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ mchezaji bora dhidi ya Sudan Kusini na Stumai Abdallah, ambaye atakosa mashindano ya msimu huu kwa sababu yupo kozi ya ajira ya JWTZ alikuwa mchezaji bora dhidi ya Zimbabwe.
MSIMU HUU
Twiga Stars imepangwa Kundi C pamoja na timu za Malawi, Comoro na Botswana, ambao walikutana nao pia msimu uliopita na Kundi A lina mwenyeji Afrika Kusini, Msumbiji, Angola na Mauritius na Kundi B lina timu za Lesotho, Zambia, Eswatini na Namibia.
Kwa mujibu wa ratiba nusu fainali, mshindi wa Kundi B atacheza na mshindi wa Kundi C na mshindi wa Kundi A atacheza na mshindwa bora na fainali zitachezwa Septemba 11,
hivyo mshindi wa kwanza kila kundi ndio watafuzu nusu fainali.
Hata hivyo, wachezaji wa Twiga Stars wana ari ya kufanya vizuri ikichagizwa na viwanja walivyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita.
Nahodha wa Twiga Stars, Amina Bilali anasema wako tayari kuonesha hawakubahatisha kufika fainali bila kufungwa na kutwaa ubingwa uliomfurahisha Rais Samia na kuwapa viwanja jijini Dodoma.
“Tunataka Mama Samia ajue kuwa hatukubahatisha tupo tayari kutetea ubingwa wetu tuendelee kuonesha kuwa wanawake wanaweza kama yeye anavyotuongoza akiwa
mwanamke wa kwanza Tanzania kuwa Rais,” alisema Amina.
SHIME ALONGA
Kocha timu za soka za Taifa za wanawake, Bakari Shime anasema anaamini Twiga Stars itakwenda kutetea ubingwa wa mashindano ya Cosafa kwa namna ambavyo wamejiandaa.
“Tumefanya maandalizi mazuri na tutaanza kurusha karata ya kwanza kwa kucheza na Comoro na Septemba 2 na nina imani tutatetea ubingwa maana sisi ndio mabingwa
watetezi,” alisema Shime.
Alisema watahakikisha wanashinda michezo yote katika hatua ya makundi maana mshindi wa kwanza tu ndio wanafuzu nusu fainali na timu ya nne itakuwa mshindwa bora.
Baada ya mchezo dhidi ya Comoro, Twiga Stars mchezo wa pili itavaana na Botswana Septemba 5 na watamaliza hatua ya makundi Septemba 7 kwa kucheza na Malawi, ambao
walicheza nao fainali msimu uliopita.
TIMU ZINGINE
Mwishoni tu mwa mwaka 2018, timu ya Taifa ya Wasichana chini ya umri wa miaka 17 ndio ilikuwa bingwa wa mashindano hayo kwa umri huo, ambapo pia mwaka mmoja nyuma (2019) timu ya Taifa ya Tanzanite (U-20) nao walichukua ubingwa kwenye mashindano hayo.