Kwingineko

Drake aisaidia Venezia kupata uwekezaji Serie A

ROME: RAPA maarufu wa Canada Aubrey Graham ‘Drake’ ameisaidia klabu ya Venezia FC ya nchini Italy kupata uwekezaji mkubwa kutoka kwa mfanyabiashara wa michezo Tim Leiweke.

Venezia ambayo imefanikiwa kurejea katika ligi kuu ya Italy, Serie A msimu huu, imetangaza kupokea uwekezaji wa euro milioni 100 sawa na zaidi ya Sh bilioni 300 za Kitanzania.

Drake ambaye alijiunga kama mwekezaji wa Venezia mwaka 2024, ametajwa kusaidia kumleta Leiweke pamoja na Francesca Bodie kuwekeza kwenye klabu hiyo.

Leiweke ni mmoja wa viongozi maarufu katika sekta ya michezo Marekani akiwa amewahi kufanya kazi na timu mbalimbali za NBA, NHL na MLS zikiwemo LA Galaxy, Los Angeles Lakers pamoja na Toronto Maple Leafs.

Kupitia uwekezaji huo, Leiweke ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mwenza wa kamati ya uendeshaji ya Venezia huku Francesca Bodie akichukua nafasi ya rais wa klabu hiyo.

“Tunaamini Venezia ni klabu yenye historia kubwa katika moja ya miji mizuri zaidi duniani na tutapambana kuhakikisha tunajenga utamaduni wa ushindi pamoja na kuwapa mashabiki uzoefu wa kiwango cha dunia,” amesema Leiweke.

Venezia imepanda Serie A baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Spezia Calcio, na kurejea ligi kuu msimu mmoja tu baada ya kushuka daraja mwaka 2025.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button