Simeone ajivunia Atlético Licha ya kutolewa na Arsenal

LONDON: KOCHA Mkuu wa Atletico Madrid, Diego Simeone, ameonesha kujivunia kiwango cha timu yake licha ya kutolewa kwenye nusu fainali ya UEFA Champions League kufuatia kichapo kutoka kwa Arsenal Jumanne usiku.
Simeone alikiri kuwa wapinzani wao walistahili kusonga mbele, akieleza kuwa walikuwa makini zaidi hasa kipindi cha kwanza, jambo lililowapa faida muhimu. Hata hivyo, alisisitiza kuwa timu yake ilipambana kwa kiwango cha juu licha ya kushindwa kutumia nafasi walizopata.
“Kama tumetolewa ni kwa sababu wapinzani walistahili kusonga mbele. Walikuwa makini kipindi cha kwanza. Lakini najisikia utulivu, timu ilitoa kila kitu. Tulipaswa kushinda mechi ya kwanza lakini hatukuwa makini vya kutosha,” amesema Simeone.
Kocha huyo pia amegusia tukio tata la penalti iliyodaiwa kufanywa dhidi ya Antoine Griezmann, akisema tukio hilo lilikuwa wazi lakini hawataki kulitumia kama kisingizio cha matokeo.
Mbali na hilo, Simeone ameeleza kuwa timu yake ilikumbwa na changamoto ya kushindwa kutumia nafasi muhimu.
Aidha, amedokeza tofauti ya rasilimali kati ya timu hizo mbili, akimsifu kocha wa Arsenal Mikel Arteta kwa kazi kubwa anayoifanya huku akigusia uwezo mkubwa wa kifedha wa klabu hiyo.
“Wamefanya kazi kubwa na wana rasilimali kubwa za kifedha zinazowawezesha kufika hapa walipo,” amesema.
Licha ya kutolewa, Simeone amesisitiza kuwa safari yao ya Ligi ya Mabingwa ilikuwa ya mafanikio makubwa, hasa kwa kufika hatua ambayo wengi hawakuitarajia huku akiwapongeza mashabiki wa Atlético Madrid kwa sapoti kubwa waliyoitoa, akisema timu ilifanya kila iwezalo na ilistahili angalau kupata nafasi ya kucheza muda wa nyongeza.




