Dembélé amtaja Gavi baada ya kuimaliza Bayern

MUNICH: NYOTA wa Paris Saint-Germain, Ousmane Dembélé, ameibua gumzo mitandaoni baada ya kusherehekea kufuzu kwa timu yake hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kushiriki video ya kiungo wa Barcelona, Pablo Martin ‘Gavi’, kwenye akaunti yake ya mtandaao wa kijamii.
PSG imefanikiwa kufuzu fainali hiyo itakayochezwa Budapest baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Bayern Munich, na kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 6-5 katika hatua ya nusu fainali.
Katika video hiyo, Dembélé alimrejelea Gavi akijibu kauli kali aliyowahi kuitoa kuhusu wakosoaji wake, akisisitiza kuwa watu wengi hawana uelewa wa kiwango chake cha soka.
Kauli hiyo imekuwa ikizungumzwa sana kutokana na mtindo wa moja kwa moja wa Gavi kujibu wakosoaji.
Uhusiano kati ya Dembélé na Gavi unaonekana kuwa wa karibu, kwani wawili hao waliwahi kuwa na uhusiano mzuri wakati Dembélé akiwa Barcelona, ambapo Gavi alikuwa akiibuka kikosini chini ya kocha Ronald Koeman.
Inaripotiwa pia kuwa Gavi aliwahi kumshawishi Dembélé asiondoke Barcelona mwaka 2023 kabla ya kujiunga na PSG.
Dembélé, ambaye sasa anang’ara akiwa PSG, amekuwa akionekana kuwa katika kiwango bora zaidi hasa katika hatua za mwisho za msimu wa Ligi ya Mabingwa.




