Kwingineko

Vini ‘moto’ Real ikiifumua Salzburg

PHILADELPHIA, Mshambuliaji wa Real Madrid Vinícius José Paixão de Oliveira Júnior maarufu Vinicius Jr alifunga bao moja na kutengeneza jingine wakati klabu yake ikipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya RB Salzburg alfajiri ya leo na kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia la Klabu wakiwa kileleni mwa Kundi H.

Wahispania hao wamekamilisha hatua ya makundi wakiwa na pointi saba, mbili mbele ya Al-Hilal ya Saudi Arabia, ambao waliifunga Pachuca mabao 2-0 katika mechi nyingine ya kundi hilo. Salzburg ya Austria yenye pointi nne, na Pachuca ya Mexico ambayo ilishindwa kupata hata pointi moja wameondolewa mashindanoni.

Real Madrid ya Xabi Alonso iliutawala mchezo huo dhidi ya Salzburg, ambao walitengeneza nafasi chache za wazi. Kipa wa Salzburg, Christian Zawieschitzky, mwenye umri wa miaka 18, alijizatiti vyema langoni tangu mwanzo na akimnyima Vinicius nafasi ya kufunga bao la mapema.

Fowadi huyo wa Brazil alipoteza nafasi nyingi zaidi huku Gonzalo Garcia pia akikosa nafasi ya dhahabu iliyotokana na krosi ya Vinicius. Jitihada zake hatimaye zikalipa mnamo dakika ya 40 akifunga bao safi lililotokana na asisti ya straa mwenzake Jude Bellingham.

Vinicius aliendelea kuwa mchezaji muhimu kwenye mchezo huo akijitwisha jukumu muhimu katika bao la pili la Real katika dakika za nyongeza kipindi cha kwanza, akiokota mpira uliozagaa ndani ya eneo la hatari na kutoa pasi ya kisigino kwa Federico Valverde, ambaye alifunga.

Real Madrid waliendelea kudhibiti kipindi cha pili cha mchezo huo lakini waliendelea kupoteza nafasi mbele ya lango na haikuwa hadi dakika ya 84 ambapo Gonzalo Garcia alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la RB Salzburg.

“Tulikuwa nzuri. Tumecheza vizuri sana katika kipindi cha kwanza, lakini tulipoa kidogo kipindi cha pili. Hilo ni jambo la kawaida kwa sababu ni lazima tutazame pia mechi zinazokuja ambapo hatuwezi kumudu kuteleza. Nimefurahishwa sana na bao na asisti nilotoa. Lakini sasa inakuja sehemu muhimu zaidi, hatua ya 16 bora, na tumejiandaa” Vinicius aliiambia DAZN.

Real Madrid itamenyana na washindi wa pili wa Kundi G Juventus Jumanne saa 4 usiku kwenye Uwanja wa Hard Rock mjini Miami, huku Al-Hilal ikimenyana na Manchester City mjini Orlando alfajiri ya siku hiyohiyo.

Related Articles

Back to top button