Iniesta atua uarabuni

KIUNGO wa zamani wa Barcelona, Andres Iniesta amesaini kukipiga katika klabu ya Emirates inayoshiriki Ligi ya Kulipwa ya Muungano wa Falme za Kiarabu(UAE).
Mhispania huyo aliondoka timu ya Vissel Kobe ya Japan Julai 1, 2023 katikati ya msimu wa ligi kuu ya nchi hiyo, J-league.
Iniesta mwenye umri wa miaka 39 amecheza michezo 134 katika timu hiyo ya Japan akishinda Kombe la Mfalme mwaka 2019 na Super Cup Japan mwaka uliofuata.
Klabu ya Emirates ambayo imepanda daraja kucheza Ligi Kuu ya UAE msimu uliopita imeandika katika mitandao yake ya kijamii: ‘Karibu Iniesta’.
Iniesta alihamia Japan baada ya kuitumikia Barcelona kwa miaka 22 ambako alishinda mataji 32 akicheza mechi 674.
Alicheza michezo 133 timu ya taifa ya Hispania na kusaidia timu hiyo kushinda Kombe la Dunia 2010 na ubingwa wa Ulaya mwaka 2008 na 2012.
Timu yake mpya itaanza kampeni ya Ligi Kuu ya Muungano wa Falme za Kiarabu Agosti 19 dhidi ya Wasl.