Curry avunja rekodi NBA

SAN FRANCISCO: STEPHEN Curry ameweka rekodi mpya ya NBA baada ya kufunga mipira ya nje nane mfululizo bila kukosa kwa mara ya kwanza katika maisha yake, akimaliza mchezo na alama 30 na pasi 10 za mabao. Golden State Warriors waliibuka na ushindi wa kishindo wa 139-105 dhidi ya Philadelphia 76ers katika mchezo uliochezwa San Francisco.
Kwa kufanya hivyo, Curry, mwenye umri wa miaka 36, ameingia katika vitabu vya historia ya NBA. Ameweka rekodi mpya ya kipekee kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga angalau mipira ya nje nane bila kukosa na bado kufikisha pasi 10 za mabao katika mchezo mmoja. Ingawa rekodi ya kufunga mipira ya nje tisa mfululizo bado inashikiliwa na wachezaji wengine, kama Latrell Sprewell (2003) na Jalen Brunson (2023), Curry amejitofautisha kwa kuongeza ufanisi wake wa kutoa pasi za mabao.
Ushindi huu umeboresha rekodi ya Warriors ambapo sasa wanashika nafasi ya 9 kwenye msimamo wa ukanda wa Magharibi wakiwa wamecheza michezo 33, wakishinda 17 na kufungwa 16 msimu huu, huku 76ers wakifungwa michezo 19 na ushindi wa michezo 13 kwenye mechi 32 walizocheza.
–
Katika mchezo huo, Jonathan Kuminga alichangia alama 20 kutoka benchi, wakati Draymond Green, Andrew Wiggins, na Dennis Schroder kila mmoja alifunga alama 15.