Muziki

EAGMA msimu wa pili wazinduliwa

......wadau watakiwa kupendekeza wasanii

DAR ES SALAAM: Waandaaji wa Tuzo za East Africa Gospel Music Awards (EAGMA) wamezindua rasmi msimu wa pili wa tuzo hizo, huku wakiwataka wadau wa muziki wa injili kuanza kupendekeza majina ya wasanii wanaostahili kuwania tuzo katika vipengele mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa EAGMA, Magreth Chacha, amesema mafanikio yaliyopatikana katika msimu wa kwanza yamechochea maboresho yatakayoongeza ubora na ushindani wa tuzo hizo mwaka huu.

Amesema katika msimu uliopita, wasanii wa Tanzania walifanya vizuri kwa kutwaa tuzo nyingi, hali iliyoongeza matarajio ya ushindani mkali katika msimu wa pili.

“Tumepata mafanikio makubwa kupitia tuzo za mwaka jana. Wasanii wa Tanzania walifanikiwa kushinda tuzo nyingi, jambo ambalo linatupa wajibu wa kuboresha zaidi tuzo hizi mwaka huu,” amesema Magreth.

Ameeleza kuwa lengo la EAGMA ni kuinua hadhi ya muziki wa injili nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, pamoja na kuongeza thamani ya kazi na vipaji vya wasanii wa muziki huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa COSOTA, Victor Tesha, amesema kuendelea kufanyika kwa tuzo hizo ni hatua muhimu katika kukuza na kuthamini muziki wa injili, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda haki za wasanii na kuwapa fursa ya kutambulika katika jukwaa la kimataifa.

Msimu wa pili wa EAGMA unatarajiwa kuwakutanisha wasanii wa muziki wa injili kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki katika ushindani unaolenga kutambua ubunifu, vipaji na mchango wao katika maendeleo ya tasnia ya muziki wa injili.

Related Articles

Back to top button