Kikapu

Dar City yawakumbuka watoto ikirejea kutoka Rwanda

DAR ES SALAAM: TIMU YA Dar City Basketball Club imetoa msaada wa vyakula kwa Watoto wenye uhitaji maalum mara baada ya kurejea Dar es Salaam ikitokea nchini Rwanda ilikokuwa kwenye mashindano ya Basketball Africa League (BAL) .

Dar City iliishia hatua yar obo fainali. Katika mapokezi yao yaliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo walishiriki kutoa msaada kwenye kituo cha Watoto cha Yatima cha Ashura kilichopo Vingunguti ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutoa msaada huo Mpogolo aliwashukuru Dar City kwa sadaka hiyo na kuwapongeza kwa hatua waliyofikia.

Katika ziara hiyo, viongozi, makocha na wachezaji wa Dar City walikabidhi msaada wa vyakula na mahitaji mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho ikiwa ni sehemu ya sadaka na shukrani kwa Mungu baada ya ushiriki wao katika mashindano hayo.

Kocha wa Dar City Mohamed Mbwana amesema licha ya kushindwa kuingia hatua ya nusu fainali, timu hiyo imeiweka Tanzania katika ramani ya mpira wa kikapu Afrika.

“Tulipambana kwa nguvu kubwa sana. Hatukuweza kufanikiwa kuingia nusu fainali lakini tunajivunia kuiwakilisha vizuri Tanzania katika mashindano haya makubwa ya BAL Six,” amesema
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa na sapoti kubwa kutoka serikalini, mashabiki pamoja na wadau wa michezo nchini.
Kocha huyo alimshukuru Rais wa Klabu hiyo Musa “Mzenji” kwa uwekezaji alioufanya kwa vijana wa timu hiyo.
“Tunashukuru Watanzania wote waliokuwa nyuma yetu kutusapoti. Tunaamini mafanikio haya yatakuwa chachu ya sisi kujipanga vizuri zaidi ili mwakani turejee kwa nguvu na kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania,” amesema.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Hasheem Thabeet amesema shirikisho hilo litaendelea kuhamasisha utamaduni wa kusaidiana katika jamii huku akieleza kuwa michezo ni sehemu ya kuunganisha watu na kutoa matumaini kwa vijana.
“Huu ni utaratibu tunaotaka kuendelea nao kila mwaka katika kipindi kama hiki cha Eid ili kuonesha upendo kwa jamii,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa wa Kituo cha Ashura Foundation, Waziri Said, amewashukuru Dar City kwa msaada huo akisema umewafariji watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Amesema kituo hicho chenye watoto 24 kimekuwa kikilea watoto katika mazingira magumu huku baadhi yao wakiwa tayari wamefikia hatua za elimu ya juu.
“Kituo chetu kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania na tunashukuru sana kwa msaada huu. Tunawaombea Dar City waendelee kufanya vizuri zaidi na kuiwakilisha Tanzania kimataifa,” alisema.
Aidha, aliomba wadau wa michezo kuendelea kusaidia watoto wenye vipaji vya mpira wa kikapu ili waweze kufikia ndoto zao.

Related Articles

Back to top button