Clara Luvanga: Nidhamu huleta ushindi
SAUDI ARABIA: NYOTA wa Twiga Stars anayekipiga Al Nassr FC ya Saudi Arabia Clara Luvanga amesema nidhamu binafsi ni muhimu ili kuishi maisha ya ushindi.
Kauli yake hiyo inakuja baada ya kuisaidia timu yake kushinda mabao 2-1 dhidi ya Al Amal jana huku Clara akifunga bao moja.
Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii nyota huyo aliweka ujumbe leo akisema nidhamu ni muhimu sana kwani inamsaidia kuona baraka za Mungu.
“Nidhamu binafsi ni kitu muhimu sana uweze kuishi maisha ya ushindi na kuona baraka za Mungu,”aliandika ujumbe huo kueleza siri ya mafanikio yake kwa kile anachokifanya.
Ubora wa kiwango chake katika klabu hiyo kubwa Saudi Arabia umempa nafasi ya kuaminika kwenye kikosi cha kwanza na kuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo.
Mbali na Clara anayekipiga nje ya nchi, wengine ni Hasnath Ubamba ambaye pia, aliiwezesha timu yake ya FC Masar ya Misri kupata ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ittihad Bassioun. Katika mchezo huo Hasnath alifunga mabao mawili. Pia, kuna Opa Clement anayekipiga China na Jullita Singano Mexico.