Ratcliffe atuhumiwa kuivuruga Man U

MANCHESTER, Nyota wa zamani wa mashetani wekundu Manchester United, Eric Cantona amemtuhumu mmiliki mwenza wa klabu hiyo Sir Jim Ratcliffe na wasaidizi wake kuiharibu na kuiangamiza klabu hiyo yenye maskani yake viunga vya Trafford jijini Manchester.
Mshambuliaji huyo aliyeisaidia United kutwaa ubingwa wa Ligi mwaka 1993 amesema haridhishwi na namna klabu yake hiyo ya zamani inavyoendeshwa chini ya Sir Jim akisema ikiwa mwekezaji huyo ataendelea kusalia klabuni hapo United itakuwa pabaya zaidi.
“Tangu Ratcliffe atue United na timu hii ya Wakurugenzi wanajaribu kuvuruga kila kitu na hakuna mtu yeyeote wanamuheshimu. yani wanataka hata kubadilisha uwanja wakati timu haina ari ya uchezaji”.
“Lazima wajue watu wanaoizunguka United ni kama Familia kubwa ni ,muhimu sana kuwaheshimu kama unavomheshimu kocha na wachezaji. Tangu afike ni tofauti sana hamtaki tena Sir Alex Ferguson kama balozi wa United hazingatii maoni yake” – Cantona Mewaambia waandishi wa habari katika tukio la timu ya daraja la chini iliyoanzishwa na mashabiki ya FC United.
Bilionea Mwingereza Sir Jim Ratcliffe amekuwa na misukosuko mingi tangu aanze kushughulika moja kwa moja na uendeshaji wa United baada ya kununua hisa mwaka 2024. mmiliki huyo wa INEOS alimfuta kazi Erik ten Hag na kumleta Ruben Amorim ambaye mpaka sasa yupo nao nafasi ya 13 ya Ligi.
Shabiki huyo wa utotoni wa United pia alipandisha bei za tiketi za mechi za klabu hiyo na kuleta sera za kubana matumizi zilizosababisha upotevu wa karibu ajira 450 huku akitangaza mpango wake wa kujenga uwanja mpya wa klabu hiyo uliopokelewa kwa hisia tofauti.