CEO Bodi ya Ligi asisitiza ubora wa viwanja Ligi kuu bara

DAR ES SALAAM: WAKATI Ligi Kuu ya NBC Tanzania inatarajia kuanza Agosti 16, mwaka huu, ofisa tendaji Mkuu wa Bodi ligi kuu Tanzania Bara (TPLB), Almas Kasongo amesema msimu wa 2024/25 wanakuwa wakali zaidi katika sheria namba moja kati ya 17 za soka inayozungumzia miundombinu ya kuchezea soka.
Amesema msimu uliopita walikutana na changamoto kubwa ya uwanja na safari hii wamezingatia mambo matatu muhimu ikiwemo sehemu ya kuchezea (Pitch), jukwaa la kukaa mashabiki wasiopungua elfu (3000) na sehemu ya kisasa ya kukalia benchi la ufundi.
Ofisa Mtendaji wa TPLB, Kasongo ameiambia Spotileo kuwa, kutokana na changamoto walizokutana nazo kwa kufungia viwanja vingi ambavyo havikukidhi vigezo, msimu wa 2024/25, wapo makini kuhakikisha mechi zinachezwa kwenye viwanja bora.
“Ni kweli msimu uliopita ilikuwa changamoto kubwa,safari hii hatutataka yatokee tena msingi wake tunahitaji kusimamia ligi zetu tatu kuhakikisha zinachezwa katika viwanja vinavyokidhi katika sheria namba moja kati ya 17 za soka.
Tunatambua ligi Tanzania ilikuwa nafasi ya tano bora Afrika na kushuka hadi sita, lakini tunahitaji kuwa bora zaidi lazima tusimamia vizuri miundo mbinu ikiwemo uwanja kwa lengo la kuvutia wadhamini, makocha na wachezaji wakigeni,” amesema Kasongo.
Kuhusu teknolojia ya teknolojia ya usaidizi wa muamuzi kwa njia ya video VAR kutumika kwenye michezo miwili ya Ngao ya Hisani, Kasongo amesema haiwezi kwa sababu kuweza kutumia kifaa hicho hadi kupata kibali kutoka Shirikisho la Soka Ulimwengine (FIFA) na Afrika (CAF).
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) anaendelea na mchakato wa kufatilia kibari na leo jioni walikuwa na kikao kwa njia ya mtandano na watu wa FIFA na CAF kujadiliana suala hilo na lini tutapewa kibali hicho na baadae tutaangalia kuwajenga uwezo waamuzi wetu jinsi ya kutumia VAR, bahati nzuri vifaa tunavyo,” amesema Kasongo.
Kutokana na mchakato huo wa kuendelea kuomba kibali kuna uwezekano wa mechi za Ngao Hisani itachezwa bila ya kuwepo kwa kifaa hicho, michezo hiyo itakayochezwa, Agosti 8, mwaka huu, Benjamini Mkapa, Dar es Salaam na New Aman Complex, Visiwani Zanzibar