Cassie:Lucy Komba ndiye alinifundisha kiswahili

MSANII wa filamu kutoka nchini Zambia, Cassie Kabwita amesema mwigizaji mkongwe Lucy Komba ndiye aliyemsaidia kujifunza lugha ya Kiswahili pamoja na uigizaji alipokuwa akiendeleza safari yake ya sanaa nchini Tanzania.
Cassie ambaye ameonekana katika kazi mbalimbali za filamu na tamthilia Tanzania, amesema Lucy Komba alikuwa mwalimu wake mkubwa katika hatua za mwanzo za kazi yake ya sanaa hapa nchini.
“Nimeamua kurudi nyumbani kwa mwalimu wangu wa Kiswahili, Lucy Komba.
‘Acting coach’ wangu, sasa hivi ananifundisha Kidenish. Thank you very much sweet Jesus for making us meet again in good health, I love you dada,” ameandika Cassie katika sehemu ya ujumbe wake akionesha kuthamini mchango wa Lucy Komba katika maisha yake ya kisanii.
Cassie Kabwita ambaye ana takribani miaka 20 katika tasnia ya uigizaji, alianza kupenda sanaa tangu akiwa mdogo.
Alikuwa akimchukulia mwigizaji wa Nigeria, Omotola Jalade Ekeinde kama kioo chake cha mafanikio kutokana na kazi zake mbalimbali za filamu.
Ndoto yake ilitimia mwaka 2018 baada ya kukutana naye uso kwa uso katika hafla ya Africa Magic Viewers’ Choice Awards.
Mbali na Zambia, Cassie ameigiza filamu katika mataifa mbalimbali ya Afrika ikiwemo Nigeria na Ghana.
Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania alimpongeza pia mwigizaji Jacob Stephen maarufu kama JB kwa mchango wake katika kukuza kipaji chake kupitia kazi walizocheza pamoja kama Vita Baridi, Mzee wa Swaga na tamthilia ya Mzani wa Mapenzi.
Kwa upande wake, Lucy Komba ana zaidi ya miaka 26 katika tasnia ya sanaa nchini Tanzania.
Alipata umaarufu kupitia tamthilia za kundi la Kaole kabla ya kuendelea kung’ara katika filamu mbalimbali, nyingi akiwa mtayarishaji wake mwenyewe.
Mbali na uigizaji, Lucy pia amewahi kuwa mwandishi na muongozaji wa filamu ambapo aliwasaidia wasanii wengi chipukizi kupata nafasi ya kuonekana na kukua kisanaa, wakiwemo Jacqueline Wolper, Irene Uwoya, Irene Paul na Yusuph Mlela pamoja na wengine wengi.
Kwa takribani miaka 10 sasa, Lucy Komba anaishi nchini Denmark alikohamia baada ya kuolewa na mumewe raia wa nchi hiyo.




