Tamasha la Sauti za Busara 2025 kufanyika leo Zanzibar

ZANZIBAR: TAMASHA la 22 la Kimataifa la Muziki la Sauti za Busara kwa mwaka huu wa 2025 linatarajiwa kuanza kufanyika leo Februari 14 hadi 16 katika Mji Mkongwe, Zanzibar.
Tamasha hilo la muziki wa ‘LIVE’ litawakutanisha wasanii kutoka mataifa mbalimbali duniani kote ambao wataonesha uwezo katika majukwaa matatu tofauti mawili ndani ya Ngome Kongwe, na jukwaa lingine litafungwa nje, Forodhani.
Mkurugenzi wa tamasha hilo, Journey Ramadhan ameiambia SpotiLeo kuwa mipango yote imekamilika na tamasha hilo litaanza kwa maandamano yatakayoongozwa na makundi mbalimbali yakiashiria ufunguzi wa tamasha hilo la siku tatu visiwani hapo.
Amesema tamasha hilo ni kichocheo cha kuongeza ajira kwa Wazanzibar na pia kuongeza Uchumi wa Zanzibar kwa ujumla kupitia utalii kutokana na idadi kubwa ya watalii waliopo Zanzibar kwa kipindi chote cha tamasha hilo.
Mwanamuziki Christian Bella na Frida Amani ni miongoni mwa wasanii kutoka Tanzania bara watakaotumbuiza katika tamasha hilo huku wasanii na vikundi vya ngoma za asili kutoka Zanzibar na nje ya Zanzibar vikitarajiwa kuwa sehemu ya burudani katika tamasha hilo la siku tatu.