CAF yaridhishwa miundombinu ya viwanja Arusha

ARUSHA:WAJUMBE wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana walifanya ziara ya ukaguzi wa miundombinu katika viwanja vya Arusha vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON 2027.

Katika ziara hiyo, ujumbe huo ulikagua maeneo mbalimbali ya Uwanja wa Arusha, ikiwemo mifumo ya usalama, maeneo ya watazamaji, huduma za kibiashara pamoja na maeneo mengine muhimu yanayohusiana na uendeshaji wa mashindano hayo.
Aidha, CAF ilikagua viwanja vya mazoezi vya Mgambo, Engutoto na Magereza, pamoja na vituo vya huduma za kwanza na hospitali zitakazotumika wakati wa mashindano hayo, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya utayari wa miundombinu na huduma muhimu.

Ziara hiyo ilifanyika kwa kushirikiana na Kamati ya Ndani ya Maandalizi ya AFCON 2027, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa CAF wa kuhakikisha miundombinu na huduma zote zinakidhi viwango vinavyohitajika kwa ajili ya kuandaa mashindano ya kiwango cha Afrika.
Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika Mashariki, pamoja na Kenya na Uganda, zitakazokuwa wenyeji wa AFCON 2027. CAF inaendelea na ukaguzi wa miundombinu katika nchi hizo ili kufuatilia maendeleo ya maandalizi na kuhakikisha viwango vinavyohitajika vinafikiwa.




