Kwingineko

“Brazil tunapiga hatua” – Dorival Jr

BRASILIA, Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil, Dorival Jr amesema kikosi chake kinapiga hatua licha ya kuonekana kusuasua kwenye michuano ya kusaka kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2026 na kushika nafasi ya 5 kwenye msimamo unaoongozwa na Argentina kuelekea michezo muhimu ya kufuzu michuano hiyo dhidi ya Peru na Colombia.

Mabingwa hao mara 5 wa kombe la Dunia wako kwenye shinikizo kubwa baada ya kushinda michezo miwili pekee katika michezo mitano iliyopita kufuatia muendelezo mbaya wa kikosi hicho chenye majina makubwa kwenye soka ulimwenguni.

Brazil wamepata sare ya 1-1 mara mbili mfululizo dhidi ya Venezuela na Uruguay lakini Dorival anaamini wamejipata na sasa wako tayari kurejea kwenye ushindi watakapoikaribisha Colombia katika mji mkuu wa Brasilia leo Alhamisi.

“Tunawajibika moja kwa moja na matokeo haya mabaya na kila kitu kinachotokea. Tunajipapatua kwenye mashindano ambayo kila siku yanakuwa magumu, kwakweli tunahitaji kujipanga upya tuwe na safu nzuri ya ulinzi na ushambulizi.”

“Ningekuwa na wasiwasi zaidi ya nilionao leo kama ningekuwa sioni maendeleo yoyote kwenye kikosi. Tunajitahidi kujirekebisha ili matokeo ya mchezo ujao yawe tofauti, lakini nawahakikishia kuna hatua tumepiga japo wengi hamtaki kuziona” Dorival amewaambia wanahabari

Brazil wamekuwa nje ya mazingira waliyoyazoea kwa zaidi ya miaka miwili tangu walipoondolewa na Croatia kwenye kombe la dunia la 2022 nchini Qatar jambo lilipelekea kuondoka kwa kocha wao wa muda mrefu Titte.

Dorival mpaka sasa bado hajaingia kwenye mioyo ya mashabiki wa Brazil baada ya kushinda mechi sita tu kati ya 14 aliyoiongoza timu hiyo ikiwemo Copa America waliyoondolewa na Uruguay.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button