Benfica yaongeza dau la kumbakisha Mourinho

LISBON: KLABU ya Benfica imeongeza kiwango cha fedha kinachohitajika kwa Jose Mourinho kuondoka klabuni hapo na kujiunga na Real Madrid baada ya kipengele chake cha kuachiliwa kumalizika.
Ripoti zinaeleza kuwa Real Madrid tayari imekubaliana mkataba wa miaka miwili na Mourinho ambaye anatajwa kuwa chaguo la rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, kuchukua nafasi ya ukocha msimu ujao.
Hata hivyo, mpango huo umecheleweshwa kutokana na uchaguzi wa urais wa Real Madrid unaotarajiwa kufanyika baada ya mgombea Enrique Riquelme kuthibitishwa rasmi kupambana na Perez.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kipengele cha Mourinho kuondoka Benfica kilikuwa na thamani ya euro milioni saba, lakini baada ya kumalizika kwa muda wake, Benfica sasa inadaiwa kutaka euro milioni 15 ili kumuachia kocha huyo raia wa Ureno.
Fedha hizo zinatajwa kuwa sawa na mshahara wa Mourinho ndani ya Benfica, huku ikielezwa kuwa mazungumzo yanaweza kufanyika ili kupunguza kiwango hicho ingawa haitarajiwi kushuka hadi euro milioni saba za awali.
Licha ya hali hiyo, Mourinho anaelezwa kuwa hana presha kuhusu hatma yake na bado ana matumaini makubwa ya kurejea Real Madrid kwa mara ya pili baada ya kuinoa timu hiyo miaka ya nyuma.
Hatua hiyo inaweza kuifanya Real Madrid kuongeza gharama zaidi iwapo itasubiri hadi uchaguzi ukamilike kabla ya kuthibitisha ujio wa Mourinho rasmi.




