Ben Pol kutoa wimbo wa nishati safi

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI Benard Paul ‘Ben Pol’ ametangaza kuachia video ya wimbo maalum wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ben Pol ambaye pia, ni mwanamazingira amekuwa akitumia sanaa yake ya muziki kuelimisha jamii masuala mbalimbali.
Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii, msanii huyo amesema wimbo huo ulioko chini ya mradi wa Mkombozi unatarajia kukamilika muda sio mrefu.
“Niko katika matayarisho ya video ya wimbo maalum wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia chini ya Ben Pol Foundation,”amesema nyota huyo anayefanya kazi na mashirika ya vijana ya kimataifa.
Msanii huyu hivi karibuni hajaachia wimbo wa kiushindani akionekana kubanwa na majukumu ya kazi nyingine za miradi ya kimazingira anazofanya.
Mara ya mwisho ni mwaka uliopita aliachia wimbo unaosema I’m in Love’ akishirikiana na Saraphina Michael ‘Phina’. Wimbo wake uliowahi kufanya vizuri ni Moyo mashine alioutoa miaka nane iliyopita ulifikisha zaidi ya watazamaji milioni 17 .